Kortini kwa kumchoma mtoto kwa moto wa mkaa

MKAZI wa Matalawe mkoani Njombe, Furaha Lugenge (28) amefikishwa mahakamani kwa kosa la kumchoma moto mtoto wa mume wake sehemu za mapajani na kwenye makalio kwa kutumia moto wa mkaa kwa madai ya mtoto huyo kukojoa kitandani.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Njombe, Matilda Kayombo, waendesha mashtaka wa Serikali, Tito Mwakalinga na James Lekey, walieleza kuwa Desemba 19, 2022 katika mtaa wa Matalawe Mjini Njombe, mshtakiwa wakati akifanya usafi aligundua kuwa mtoto huyo(8) anayesoma darasa la pili kakojoa kitandani na ndipo akamuadhibu kwa kumuunguza na moto wa mkaa.

Imeelezwa kuwa kosa hilo, shauri  namba 6 la mwaka 2023 ni  la kujeruhi na kinyume na kifungu namba 225 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16 marejeo ya mwaka 2022.

Upelelezi wa shauri hilo umekamilika  ukiwa na mashahidi watano na vielelezo viwili sambamba na muathirika wa tukio hilo ambaye amekiri kufanyiwa kitendo hicho.

Shauri hilo lilianza kusikilizwa mwishoni mwa wiki ambapo liliahirishwa mpaka leo baada ya mtoto huyo kushindwa kuendelea kuzungumza kutokana na kulia.

Mshitakiwa aliruhusiwa kurudi nyumbani kwake baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.

Habari Zifananazo

Back to top button