Kortini kwa kutolipa kodi

MFANYABIASHARA Emmanuel Kapaya amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Geita akituhumiwa kukwepa kulipa kodi kwa miaka saba na kuisababishia hasara serikali.

Imedaiwa ndani ya kipindi cha miaka saba kuanzia mwaka 2016 hadi 2023, mfanyabiashara huyo mwenye leseni ya benki kuu alikwepa kulipa kodi ya  jumla ya Sh 3,496,400.

Mtuhumiwa alisomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Christopher Waane na wakili wa Jamhuri, Mussa Mlawa.

Advertisement

Wakili Mlawa alisema uchunguzi bado unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atasomewa mashitaka yake kwa ridhaa ya Mkurugenzi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP).

Mawakili wa utetezi, Beatus Emmanuel na Yesse Simon walipinga madai hayo ya upande wa Jamhuri na kuieleza mahakama maelezo ya Jamhuri yanakinzana na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Wakili Beatus aliiambia mahakama kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo mtuhumiwa hakupaswa kufunguliwa kesi hiyo endapo upelelezi haujakamilika na kama hakuna ridhaa ya ofisi ya DPP.