Kortini wakidaiwa kuisababishia TRA hasara Sh Mil 592

DSM; WAKAZI wanne wa Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakikabiliwa na mashitaka sita ikiwemo kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh milioni 592.3 na utakatishaji fedha.

Washitakiwa hao ni Salum Mbegu (38) Mkazi wa Majohe Mji mpya, Peter Ntikula (27) Mkazi wa Buguruni, Baraka Ntikula (37) Mkazi wa Mkuranga na Hamad Hamad.

Washitakiwa hao walisomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Gloria Mwenda akisaidiana na Upendo Mono, Medalakini Emmanuel na Hauni Chilamula mbele ya Hakimu Mfawidhi, Susan Kihawa.

Mwenda amedai washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuongoza genge la uhalifu, kutumia mashine za kielektroniki za EFD kwa lengo la kuharibu mfumo na kumdanganya Kamishina, kutoa risiti zisizo halali za EFD, kukutwa na mali iliyoibwa au kupatikana kinyume na sheria, kuisababishia mamlaka hiyo hasara na kutakatisha fedha.

Katika mashitaka ya kwanza, Mwenda amedai kati ya mwaka 2018 na Oktoba 3 mwaka huu, maeneo ya Buguruni Kisiwani, wilayani Ilala, Dar es Salaam, kwa lengo la kujipatia faida, waliongoza genge la uhalifu kwa kutumia mashine ya EFD kuharibu mfumo, kumdanganya Kamishina na kutoa risiti zisizo halali.

Pia amedai katika tarehe hizo, washitakiwa hao walitumia mashine za EFD kwa lengo la kupotosha mfumo kwa kutoa risiti zisizo halali na kuziingiza kwenye mfumo wa TRA na kusababisha mamlaka hiyo kudaiwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Sh 592,336,714.

Imedaiwa washitakiwa hao kwa pamoja walitoa risiti bandia za EFD kwa nia ya kumdanganya Kamishna na walipa kodi kudai Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kinyume na sheria.

Katika mashitaka ya nne inadaiwa Oktoba 3, mwaka huu washitakiwa Mbegu, Ntiluka na Baraka, walikutwa na mashine tano za EFD ambazo walizipata kinyume na sheria.

Inadaiwa kati ya mwaka 2018 na Oktoba 3 mwaka huu, washitakiwa hao kwa pamoja waliisababishia TRA hasara ya Sh milioni 592.3 kwa kutoa risiti zisizo halali.

Mwenda amedai katika mashitaka ya sita ya utakatishaji fedha kuwa washitakiwa hao kwa pamoja walihusika kutoa muamala wa Sh milioni 592.3, wakati wakijua fedha hizo kuwa zao la uhalifu.

Washitakiwa hao walikana mashitaka hayo na upande wa mshitaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo, waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Kihawa amesema kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana katika kesi ya uhujumu uchumi, hivyo aliwataka washitakiwa kurudi rumande hadi Oktoba 30, mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button