Kotini wizi wa Sh bilioni 1 za benki

WAFANYABIASHARA Valentine Zacheus (42) raia wa Ghana aishiye Tanzania na Fortunatus Bundala (36) mkazi wa Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kuiba Sh bilioni 1.6, mali ya African Banking Corporation Tanzania Limited (BancABC).

Akiwasomea mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi, Wakili wa Serikali, Clemence Mango alidai kuwa washtakiwa hao katika siku tofauti kati ya Oktoba Mosi, 2021 na Julai 31, 2022 katika maeneo ya Dar es Salaam na Arusha walipanga njama ya kuiba.

Katika mashtaka ya pili katika siku tofautitofauti kati ya Oktoba Mosi, 2021 na Julai 31, 2022 katika maeneo ya Dar es Salaam na Arusha waliingilia mifumo kwa njia isiyo halali.

Katika mashtaka ya tatu katika siku tofauti kati ya Oktoba Mosi, 2021 na Julai 31, 2022 katika maeneo ya Dar es Salaam, Arusha, Ghana, Uganda na Ivory Coast washtakiwa wanadaiwa kuiba Sh bilioni 1.6 mali ya BancABC.

Wakili Mango alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa hoja za awali.

Washitakiwa walikana kuhusika na makosa yote matatu ambapo wakili upande wa utetezi, Datius Faustine aliiomba mahakama iwapatie wateja wake dhamana.
Mahakama iliwasomea masharti matatu ya dhamana ambayo ni watuhumiwa wawe na wadhamini wawili kila mmoja, wawasilishe Sh milioni 400 taslimu au hati ya kiwanja ama nyumba yenye thamani hiyo na sharti la tatu, hawatakiwi kusafiri nje ya nchi na wanatakiwa kukabidhi nyaraka zao za kusafiria polisi.

Kutokana na masharti ya dhamana waliyopewa wakili upande wa utetezi aliomba siku saba ili waweze kutimiza masharti hayo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 14, mwaka huu kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hoja za awali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button