Kroos kwenye usahihi wa nyakati, vitendo

MADRID, HISPANIA: Usahihi ni Nini?

Ni hali ambayo matokeo ya vipimo ama hesabu hupatikana na thamani sahihi kwa kiwango halisi.

Kipimo cha usahihi kwa kawaida hupimwa kwa makosa ya asilimia, ambayo huamua kwa asilimia ngapi kuna mapungufu ya usahihi katika uchunguzi uliofanywa kwenye sampuli.

Ikiwa matokeo ya kipimo ni mbali na thamani halisi basi asilimia ya kutokuwa sahihi ipo juu kuliko ile ya kuwa na usahihi.

January 04,1990 kule Greifswald, Mashariki mwa Ujerumani alizaliwa mwanadamu aliyeibeba dhana ya neno usahihi kwa vitendo na kuileta kwenye soka akionyesha ni kwa namna gani unaweza kucheza mpira bila kuvuja jasho wala kuchafua jezi akiipa uhai ile kauli ya ‘achia moja mpira sio barua’

Akiamini mpira sio lazima uende nao kwa mchezaji mwenzio au si lazima ukae nao sana mguuni watoto wa mjini wanasema ‘unao unao sana’ bali alikuwa na fikra tofauti ya kuwa mpira huagizwa na ukatii yale maagizo.

Kama usahihi ni mtu basi ukiwa unatuma hela kwa wakala hakiki jina litakuja Toni Kroos

Akiwa ameshinda mataji 32 tokea aanze kusakata kabumbu akiwa na Bayern Munich ya pale kwao Ujerumani, Los Blancos ya pale Madrid Hispania na timu ya Taifa ya Ujerumani.

Namba hazidanganyi kwasababu hazijawahi kuongea wala kusema lolote lile ila hapa kwa maestro zilisikika zikipaza sauti kuweka wazi Toni Kroos ndio mchezaji pekee kuwa na usahihi wa kupiga pasi kwa asilimia 92+ ndani ya misimu 10 mfulululizo

Kuongeza chumvi kwenye kidonda Kroos awapo dimbani ana wastani wa 94% kupiga pasi zilizofika kwa usahihi kwenye michezo 463 aliyoitumikia Real mpaka sasa.

Ile sumu ya penzi aliyoilamba Belle 9 ndio viungo huionja na yale mateso aliyopata Anna kutoka kwa Diba ndio kipimo cha maumivu yanayopatikana dimbani ukikutana na Kroos kama Wayahudi walivyopita kwenye moto ndio hivyo hivyo viungo wa timu pinzani hupitia msoto huo huo

Mathayo 19:2; “Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”

Toni Kroos ni yule ngamia aliyepenya kwenye tundu la sindano

Jumatatu ya tarehe 21 Mei 2024 Toni Kroos alitangaza kustaafu kucheza soka baada ya michuano ya Euro itakayofanyika June 2024 kwao Ujerumani, Hakika Toni amejua kuzichagua nyakati za kusema kwaheri kwa kuwa yeye mwenyewe ni miongoni mwa binadamu wenye usahihi zaidi katika matendo yao..

One of the best midfielders to grace the game of football. Danke Toni Kroos

Habari Zifananazo

Back to top button