Kuadimika kwa sukari, 26 mbaroni

msako kila kona

BODI ya Sukari imewakamata wafanyabiashara 26 katika mikoa ya Tabora na Arusha kutokana na kupandisha bei ya sukari kiholela.

Bodi hiyo ambayo inafanya msako kila kona imewakamata wafanyabiashara saba mkoani Tabora akiwemo msambazaji mkuu wa sukari Kanda ya Ziwa.

Afisa wa bodi ya sukari  kanda ya ziwa, james Mwenda amesema katika mikoa ya Tabora na Mwanza , wamekamata wafanyabiashara 19 ambao wamekuwa wakiuza  gunia la kilo 25 kwa sh 78,000 hadi 90,000.

“Bei ya sukari ikipanda inamuumiza mwananchi wa kawaida,  kwenye oda mfanyabiashara anaandika sh 90,000 lakini kwenye risiti wanaandika sh 78,000 ikifika kwa mwananchi wa kawaida wanauza sh 4500 hadi sh 5,000,”amesema

Aidha, kwa upande wa Arusha bodi ya sukari mkoani humu imetoa bei elekezi y ash 3,000 na kwamba mfanyabiashara yeyote ambaye atakwenda kinyume basi atachukuliwa hatua.

Mhandisi Ally Mwinyimanga  kutoka bodi ya sukari, amesema kupandisha bei kiholela kunaumiza mlaji na serikali haiatakubaliana.yeyote anayeuza kwa bei tofauti, atakayekwenda kinyume  serikali itamfikia na kwamba  operesheni ya kuwasaka walanguzi inaendelea.

Wakati msako wa sukari ukiendelea, kilio cha kuadimika kwa sukari nchini kimeendelea kushika kasi kila kona kutokana na uhaba mkubwa uliopo na wananchi wanapobahatisha kuipata bei yake ni kubwa kwani kilo moja ya sukari inauzwa hadi Sh.5,000 badala ya Sh.2,800.

Kutokana na kuadimika huko wananchi wa maeno mbalimbali nchini wameendelea kupaza sauti zao kwa Serikali kuona hatua inayoweza kuchukua kuhakikisha sukari inapatikana na kwa bei ambayo itakuwa rahisi kuimudu.

Katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na majiji mengine nchini sukari imegeuka kuwa bidhaa adimu na wakati mwingine hata wafanyabiashara waliokuwa nayo wanaiuza kwa kificho utadhani wanauza bangi.

Uchunguzi wa HabariLeo umebaini  sukari imeendelea kuadimika madukani kwani kati ya maduka matano unaweza kuibahatisha kwenye duka moja tu na bei yake ni kati ya Sh 4,800 hadi Sh  5,000.

Sylvia Bomani mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam anasema licha ya sukari kuwa na mahitaji makubwa lakini kwa bahati mbaya haipatikani madukani na hata inapopatikana bei yake ipo juu .

Nae, muuza duka Hamis Chaurembo maarufu ‘Big’ amesema bei kubwa ya sukari imesababisha wananchi walio wengi kushindwa kuimudu kuinunua,hivyo kusababisha malalamiko.

“Mimi hapa dukani sina, haipatikani lakini hata nikiipata kiroba ni sh 90,000 kama nikiuza nis h 5,000 manung’uniko yanakuwa makubwa sana,”amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button