LEO Septemba 13, 2022, Rais Mteule wa Kenya, Dk William Ruto, anaapishwa kuwa Rais wa Tano wa Kenya akitanguliwa na Jomo Kenyatta, Daniel Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta anayemaliza muda wake.
Kuapishwa kwa Ruto ni matunda ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Kenya, Agosti 9, mwaka huu huku akipambana vikali katika sanduku la kura dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga.
Sisi tunawapongeza Wakenya wote kwa kukamilisha mchakato huu wa kidemokrasia kwa amani na utulivu na ndio maana tunasema, hili limeonesha kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimepata ustawi mkubwa kidemokrasia.
Tunawapongeza Wakenya kwa kulinda heshima ya EAC na hasa kutambua ukweli kuwa, kufanya kosa si kosa, bali kurudia kosa na hivyo kutoruhusu uchaguzi wa kisiasa kumwaga damu ya Wakenya kama ilivyotokea mwaka 2007.
Kwetu sisi, kuapishwa kwa Ruto leo, kunahitimisha mchakato wa uchaguzi huo na kuanza zama mpya za kuipeleka Kenya katika hatua nyingine ya maendeleo kwa kuendeleza alipoishia Uhuru Kenyatta.
Tunamtakia kila la heri Rais Mpya wa Kenya tukisisitiza na kumwombea hekima nyingi zaidi katika uongozi wake ili awaunganishe Wakenya wote kuwa wamoja dhidi ya ukabila, udini, umajimbo na ugonjwa wa chuki zinazotokana na tofauti za kisiasa.
Kadhalika, tunahimiza na kuwaomba Wakenya wa kada zote kusahau na kuzika tofauti zilizokuwapo wakati wa kampeni ama ziwe za kisiasa, kidini au kikabila na badala yake, waunganishe nguvu kuijenga Kenya na EAC huku wakianza maandalizi ya kistaarabu kwa mujibu wa sheria na taratibu kwa ajili ya uchaguzi mwingine.
Tunasema hayo kwa kuwa tunajua kwa dhati kuwa ustawi wa Kenya au nchi yoyote ya EAC ndio ustawi wa Tanzania na ndio ustawi wa EAC na Afrika kwa ujumla.
Tunapompongeza Ruto, tunamwomba aendeleze mazuri yote yaliyoanzishwa na watangulizi wake wote na pia pale waliposhindwa kukamilisha au kufanya kwa ‘ubora’ na matarajio ya Wakenya na wanaEAC, basi afanye marekebisho.
Kwetu sisi, mazuri anayopaswa kuendeleza ni pamoja na kuimarisha amani na usalama nchini Kenya, kuimarisha uanachama na ushirikiano baina ya nchi majirani zake na wanachama wa EAC pamoja na kuchangia kwa hali na mali maendeleo ya EAC katika nyanja zote yaani kisiasa, kijamii, kiuchumi, kiulinzi na usalama, kiutamaduni na hata kiteknolojia.