Kuboreshwa Bandari Kigoma kutachochea biashara

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa ujenzi wa gati la kuegeshea boti kubwa katika bandari ya Kibirizi mkoani Kigoma unatarajia kuchochea biashara baina ya Tanzania na nchi za ukanda wa maziwa makuu.

WAZIRI Mbarawa amesema hayo alipofanya ziara ya siku moja kutembelea bandari za Kibirizi na Ujiji mkoa Kigoma akiwa kwenye ziara ya siku tatu mkoani Kigoma na kubainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo utaongeza maradufu usafirishaji wa shehena na abiria kwenda kwenye nchi hizo sambamba na kuongeza mapato ya serikali.

Amesema kuwa nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) zinazotumia bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kupitisha shehena zao kutoka nje ya nchi, zimekuwa zikitumia bandari za mkoa Kigoma kupeleka bidhaa na shehena zao katika nchi hizo.

Advertisement

Katika salamu zake kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wa shehena kutoka DRC na Burundi wanaotumia bandari ya Dar es Salaam na bandari za ziwa Tanganyika, aliwataka wategemee kuboreshwa kwa kiasi kikubwa kwa utoaji huduma sambamba na kupunguza muda wa kushusha na kupakia shehena, hivyo wasafirishaji watatumia siku chache katika kushusha na kupakia shehena.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Kijavara (kulia) ,akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (katikati) kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bandari ya Kibirizi mkoani Kigoma (Picha zote na Fadhil Abdallah).

Akizungumza katika ziara hiyo Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa bandari, Mhandisi Juma Kijavara alisema kuwa uboreshaji wa bandari za mkoa Kigoma utaiwezesha mamlaka hiyo, kuongeza mapato yake kwa kiasi kikubwa kutoka kiasi cha shilingi bilioni  nane kilichokusanywa mwaka wa fedha uliomalizika.

Kijavara alisema kuwa bandari za Ziwa Tanganyika ndiyo uti wa mgongo wa usafirishaji wa shehena wa bandari ya Dar es Salaam, ambapo asilimia 96 ya shehena hizo zinaenda nchi za ukanda wa maziwa makuu Burundi, DRC huku kukiwa na ongezeko kubwa la mizigo na abiria kupitia bandari hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Kigoma,Salum Kalli amesema kuwa wanafarijika kwamba utekelezaji wa mradi huo una manufaa makubwa kwa mkoa huo, kwani kuongezeka kwa kiwango cha shehena na abiria kuna faida kubwa katika kuongeza mzunguko na mapato ya mkoa huo, lakini usalama wa vyombo vya majini wakati wa upepo na mawimbi makubwa, hivyo vyombo  na mali zao zitakuwa salama.

Awali Meneja wa mradi huo, Elly Dismass Mtaki kutoka TPA alisema kuwa mradi wa uboreshaji wa bandari za Kibirizi, Ujiji na jengo la Utawala katika bandari ya Kigoma unaogharimu shilingi Bilioni 32 umefikia asilimia 83, ambapo utekelezaji wa  mradi huo unahusisha uboreshaji wa bandari ya Kibirizi, bandari ya Ujiji na jengo la utawala la mamlaka ya bandari Kigoma.

11 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *