Kuhakiki namba za simu mwisho leo

Kuhakiki namba za simu mwisho leo

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema leo ni mwisho wa uhakiki wa namba za simu hivyo Watanzania wafanye hivyo kabla ya saa 10 jioni.

Aidha, Msigwa alisema kwa Watanzania ambao wako nje ya nchi laini zao zitafungwa na kwamba watakaporudi watatakiwa kuzihuisha.

Msigwa aliyasema hayo jijini Mwanza jana alipozungumza na waandishi wa habari kuwapa taarifa kuhusu shughuli za serikali.

Advertisement

Alisema lengo la uhakiki wa laini hizo ni kwa ajili ya kupambana na uhalifu mtandaoni ambao husababisha watu kutapeliwa na kuibiwa.

“Leo ndio mwisho wa uhakiki wa laini, kazi hiyo si ngumu kwani ukibonyeza namba *106# kisha fuata maelekezo utaweza kuhakiki namba yako na kujua kama kitambulisho chako cha taifa limetumika kusajili laini ngapi ambazo hazifahamiki ili hatua stahiki zichukuliwe ikiwemo kufungiwa,” alisema Msigwa.

Alisema baada ya uhakiki wanategemea kupata laini zilizokuwa zinatumika kutapeli na wahalifu ili waweze kuwachukulia hatua za kisheria na kuhadharisha matapeli kwamba hawatakuwa salama.

Msigwa alisema mpaka sasa watu wengi wamekamatwa kutokana na makosa ya kutapeli mtandaoni na wengine wamechukuliwa hatua.

“Serikali inaendelea na miradi mbalimbali ya kuhakikisha uchumi kidigitali na kusambaza mkongo wa taifa ili huduma za data ziwe maeneo yote nchini. Hii itasaidia wananchi kupata fursa ya kutafuta bidhaa kutoka maeneo mbalimbali,” alisema.

Msigwa alisema Tanzania ni kati ya nchi 10 zenye gharama nafuu za bando za intaneti na kwamba kilichosababisha gharama za bando kupanda ni kutoratibiwa kwa ushindani.

Alisema hakukuwa na viwango vizuri vya vifurushi hivyo kuathiri uwekezaji na kwamba baada ya serikali kuona hatari iliyopo katika uchumi, waliamua kuangalia upya suala hilo.

“Bado serikali inaangalia namna ya kushusha viwango vya vifurushi ili kubainisha kwani uchumi wa kidigitali unategemea zaidi vifurushi hivyo msiwe na wasiwasi,” alifafanua.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *