‘Kukaimu nafasi isizidi miezi 6’

SERIKALI imetoa maelekezo sita kwa Mameneja Rasilimali Watu wa taasisi  na idara za serikali kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyowekwa ya utumishi wa umma.

Akizungumza leo Aprili 27,2023 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa Jumuia ya Afrika katika masuala ya utawala na uongozi Chapter Tanzania (AAPAM), Katibu Mkuu  Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi amesema baadhi ya Mameneja Rasilimali watu ndio chanzo cha migogoro kwenye ofisi kutokana na kuwa na lugha zisizo na staha kwa watumishi na kutofuata miongozo iliyowekwa.

Akitoa maelekezo hayo amesema kwanza ni kuhakikisha watumishi wanaokaimishwa nafasi isizidi miezi sita wawe wameshathibitishwa na sio kuachwa muda mrefu.

Amesema, Mameneja Rasilimali watu hawashirikishi ofisi ya Rais na ndio maana wanafanya mambo yanayosababisha kulalamikiwa kwa kukaimisha watu nafasi kwa miaka mingi.

“Baadhi yenu hamuwashauri ipasavyo mabosi wenu… kukaimu haizidi miezi sita, lakini mtu anakaimishwa miaka mitano, miaka sita, barua haiji Utumishi matokeo yake  hafanyiwi vetting, mtu akikaimishwa barua yake ije Utumishi na CV (wasifu) yake.

“Mliowakaimisha wote hakikisheni barua za CV zao zinakuja utumishi, sasa nipate taarifa mtu amekaimishwa hakuna kilichofanyika baada ya hapo nitashughulika nae yeye, sio kwamba nawatisha lakini ripoti ya  CAG inatutaja sisi Utumishi ndio tunachelewesha wakati taarifa haziji utumishi, natoa agizo ukikaimisha fuata taratibu, hana sifa usimkaimishe ili kuepuka migogoro,”amesisitiza.

Amesema kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu watendaji hao muhimu kwa watumishi wa umma, hivyo ni vyema kuzingatia miongozo waliyopewa.

Pia, aliitaka Kamati ya Utendaji ya AAPAM kukamilisha mchakato wa chombo kimoja mpaka kufikia Juni 15, 2023, kwani imeonesha dalili ya kupingana kwa wanataaluma hiyo wenyewe kwa wenyewe kwa kuwepo vyama vingine.

“Naielekeza kamati ya AAPAM Chapter Tanzania  kusimamia mchakato wa uanzishaji wa jumuiya hiyo kwa ajili ya wataalamu waliopo katika watumishi wa umma  muwe chini ya mwamvuli mmoja, sio chama hiki kinasema hivi, kingine kinapinga.”

Mkomi ambaye alimuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo George Simbachawene, amesema maelekezo mengine ni kutaka wataalamu wa sekta hiyo kufanya tafiti  mbalimbali na kuja na mikakati inayoendana na mwelekeo mpya wa taaluma ya rasilimali watu na utawala katika  mapinduzi ya viwanda, kuandaa machapisho mbalimbali kuhusu taaluma ya rasilimali watu yatakayowasilishwa sehemu mbalimbali

“Lakini pia kuendesha vikao kama hivi kila mwaka, kwani mara ya mwisho kikao kama hiki kilifanyika mwaka 2015, kwa nini kwa sababu hatuko pamoja tunadaiwa ada ya Afrika, tusipokuwa hai kwenye mikutano hii hata maazimio yetu hayatatekelezeka.”

Aidha aliagiza wajumbe hao kushirikiana na ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutoa ushauri wa kuimarisha  idara ya rasilimali watu.

“Tunataraji kupata ushauri mzuri na kwa wakati kutoka kwenu vinginevyo tutajikuta sisi tunaenda njia nyingine na nyie mnaenda njia nyingine,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa AAPAM Chapter Tanzania, Laila Mavika amesema mbali na mkutano huo, lakini kutakuwa na mafunzo ya kubadilishana uzoefu na kukumbushana masuala mbalimbali ya taaluma hiyo.

“Mafunzo yatakuwa ya siku mbili leo na kesho  kutakuwa na mada mbalimbali ikiwemo udhibiti wa msongo wa mawazo,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button