‘Kula Maua’ inavyowanyonya wakulima wa ufuta Lindi

MINADA ya ufuta tayari imeshafanyika na msimu wa zao hilo kufungwa rasmi.

Takwimu kutoka kwa Ofisa Ushirika Mkoa wa Lindi, Projestus Paschal zinaonesha kuwa zaidi ya tani 43,000 za ufuta ghafi zimeuzwa katika minada 14 iliyofanyika katika msimu huu wa mwaka 2022/2023.

Mauzo hayo ya ufuta ghafi katika minada iliyofanyika mkoani Lindi, yanatajwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni 134.

Hizi ni fedha nyingi ambazo zinaweza kujenga barabara ya lami yenye urefu wa zaidi ya kilometa 130 (umbali kutoka Dar es Salaam mpaka Kibiti mkoani Pwani) kwa wastani wa kilometa moja kugharimu Sh bilioni 1.

Hata hivyo, swali la kujiuliza ni hili; katika fedha hizo, ni kiasi gani ambacho kimeingia katika mifuko ya wakulima wa zao hilo ambao kwa hakika ndiyo waliovuja jasho katika mashamba, kupanda, kufanya palizi na kuvuna?

Jawabu au majawabu ya swali hili yanayopatikana kutoka kwa wakulima wenyewe na wadau ambao wanahusika katika mnyororo mzima wa zao la ufuta. Yanatoa taswira jinsi sura ya mkulima isivyo fika wala kufahamika kwenye minada ya ufuta kutokana na biashara ya ‘Kula Maua’.

KULA MAUA NI NINI?

Ni mfumo wa ununuzi wa ufuta ambao uko katika ngazi ya kutoa maua katika kukua kwake. Ukiwa katika hatua hiyo, wafanyabiashara hutembelea wakulima shambani kwa lengo la kununua ufuta ambao bado haujakomaa.

Makubaliano hufanyika baina ya mwenye shamba na mnunuzi wa ufuta, na mara nyingi wakulima ndiyo huwafuata wafanyabiashara wakilenga kupata fedha kwa ajili ya kujikimu kwa mahitaji wakati wakisubiri msimu wa mavuno.

Ufuta ukiwa katika hatua ya kutoa maua, mnunuzi huenda shambani kwa mkulima ili kufanya tathmini ya ukubwa wa shamba na wingi wa maua kabla ya kuamua ni kiasi gani cha fedha kinachostahili kutolewa kwa mkulima husika.

Ufuta huo unaonunuliwa kwa mfumo wa kula maua, yaani kabla ya mavuno unanunuliwa kwa Sh 1,000 kwa kilo moja.

Baada ya kununuliwa, mfanyabiashara husubiri mpaka mkulima atakapovuna na kuchukua mazao husika bila kuongeza kiasi kingine cha fedha. Tangu anapouziwa maua hadi kuvuna, ufuta hukomaa na kuwa tayari kwa mavumo kati ya mwezi na nusu au miezi miwili.

Baada ya mavuno mnunuzi huchukua ufuta wake kulingana na fedha aliyompatia mkulima na yeye hupeleka ufuta huo kwa njia rasmi mnadani kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, ambako husubiri kati ya siku saba hadi 10 kulipwa fedha zake.

BEI YA SOKO

Katika minada 14 iliyofanywa na vyama vikuu vya ushirika vya Mkoa wa Lindi, bei ya juu ya ufuta ilikuwa Sh 3,184 na bei ya chini ilikuwa ni Sh 2,955 (au wastani wa Sh 3,000).

Hii ina maana kwamba waliouza ufuta wao kwa njia ya kula maua walipunjika kwa zaidi ya nusu ya thamani halisi ya ufuta katika bei ya soko, hali ambayo ni dhahiri iliwaathiri kimapato wakulima hao.

Wengi wanaouza ufuta wao katika mfumo wa kula maua huwa ni wanawake wajane na wazee ambapo hata hivyo utafiti unaonesha kati ya wakulima 10 waliouza ufuta wao kwa njia ya kula maua, wanne kati yao ni wajane wasioweza kumudu kununua chakula na mahitaji mengine kwa ajili ya familia zao.

Mmoja wao ni Halima Ismail (60), mjane na mkazi wa Kijiji cha Ruhoma, Kata ya Rutamba, Manispaa ya Lindi. Mama huyu anayeishi kwenye nyumba ndogo ya udongo na mjukuu wake wa miaka mitano (5), hana shughuli wala namna nyingine ya kujiingizia kipato zaidi ya kilimo.

Anasema kuwa analazimika kuuza ufuta wake kwa njia ya kula maua kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu na kukosa chakula katika kipindi cha masika, hivyo fedha aliyoipata hununua chakula kwa ajili ya kula na familia yake.

Naye Ramadhani Nasoro (65) mkazi wa Nihinu, Kata ya Rutamba, Manispaa ya Lindi, anasema huchukua hela ya kula maua ili kupata fedha ya kununulia dawa za shambani pamoja na chakula kinachomwezesha kupata nguvu ya kulima akiwa shambani.

“Pesa hii ni ndogo ila kwa sababu tunaipata wakati ambao hatuna kitu kabisa, sisi wakulima inatusaidia kwa kipindi kile ukiangalia mvua inanyesha kila mtu analalamika hana hela hivyo njia pekee ambayo mimi binafsi ninayoiona ya kunikomboa kipindi hicho cha kifuku (masika) ni kukopa hela kwa mfumo huo,” anasema Nasoro.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga pamoja na kukiri kufahamu kuwepo kwa biashara ya ‘kula maua’ anasema inachangiwa na wakulima wenyewe kutokuweka akiba ya fedha baada ya mauzo ya msimu mmoja, kwa ajili ya maandalizi ya msimu unaofuata.

“Wakulima wengi wanapouza mazao huwa hawakumbuki kama watakuwa tena na mahitaji ya pembejeo katika msimu unaofuata na hii si kwa msimu wa ufuta pekee bali hata wa korosho.

KAULI ZA WANUNUZI

Juma Omari (siyo jina lake halisi) mkazi wa Manispaa ya Lindi ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wanaojihusisha na ununuzi wa ufuta wa ‘kula maua’ anasema kila mwaka hutenga kati ya Sh milioni 10 na 15 kwa ajili ya kununua ufuta moja kwa moja kutoka kwa wakulima.

Anasema katika biashara hiyo ambayo hufanywa kwa makubaliano kati yake na mkulima, humuingizia faida hata mara tatu ya kiasi alichowekeza kwa wakulima wa ufuta japo inategemea na hali ya soko iliyopo kwa mwaka husika.

Omari alisema kuwa pamoja na biashara hiyo kufanyika kwa siri baina yake na mkulima husika lakini sasa wakulima wenyewe wameshajua na wanamfuata kutaka biashara hiyo.

Mwingine anayefanya biashara hiyo ni Shabani Athuman (si jina lake), anasema katika biashara hiyo zipo changamoto wanakabiliana nazo ikiwemo kufuatilia ufuta kwa wakulima kipindi cha mavuno kwani mashamba yako mbali na muda wa mavuno huwa ni uleule.

WANAOFURAHIA MAZAO

Wakati baadhi ya wakulima wakithibitisha kuuza ufuta wao kwa mfumo usio rasmi na kuendelea kupunjika kutoka kwa wanunuzi, hali ni tofauti kwa wakulima wengine ambao waliuza ufuta wao kwa njia ya stakabadhi ghalani.

Teodesia William mkulima wa ufuta, mkazi wa Wilaya Nachingwea, Lindi aliishukuru serikali kwa kusimamia vyema uuzwaji wa zao hilo la ufuta ambao umeleta tija kwa wakulima kupata bei mzuri.

Naye Amina Saidi, mkulima na mkazi wa Manispaa ya Lindi, mbali na kuishukuru serikali kusimamia vyema zao hilo na kuwafanya wakulima kupata bei mzuri aliiomba kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa ufuta ili kuongeza tija ya zao hilo.

Kwa mujibu wa Ofisa Ugani wa Kata ya Narung’ombe wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Idrisa Mpwawa, katika kuandaa shamba la ufuta mkulima hutumia si chini ya Sh 460,000 kwa ekari moja ya shamba la ufuta.

“Alisema katika hekari moja ya ufuta mkulima anaweza kuvuna kati ya kilo 600 hadi 800 japo hutegemea mbegu aliyotumia kupanda kwenye shamba lake.

MWONGOZO WA KUUZA UFUTA

Mwongozo wa msimu wa mwaka 2022/23 umezingatia mfumo rasmi wa stakabadhi ghalani unaosimamiwa na Bodi ya Usimamizi wa stakabadhi za ghala.

Lengo la mwongozo huo unaosimamiwa na Ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wa Mkoa wa Lindi, ni kutatua changamoto zilizojitokeza katika misimu iliyopita katika mfumo uliowekwa wa stakabadhi ghalani na ubora wa mazao.

Ofisa Ushirika wa Mkoa wa Lindi, Projestus Paschal anasema wasimamizi wakuu wanaoguswa moja kwa moja katika mnyororo wa uuzwaji wa ufuta ni vyama vya ushirika.

Mkoa wa Lindi una vyama vikuu viwili vya ushirika ambavyo ni Runali kinachojumuisha wakulima wa wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale na Lindi Mwambao kinachowaunganisha wakulima wa Halmashauri za Manispaa ya Lindi na wilaya za Mtama na Kilwa.

Wadau wengine ni vyama vya ushirika (AMCOS) halmashauri pamoja na ofisi ya mkuu wa mkoa chini yake ipo sekretarieti ya mkoa inayojumuisha ofisa ushirika na mrajisi wa vyama vya ushirika.

Kaimu Mrajisi wa Mkoa wa Lindi, Secilia Sostenes anataja malengo mengine kuwa ni kutatua changamoto za upatikanaji wa takwimu za mauzo, ongezeko la thamani ya mazao, usafirishaji kwa wanunuzi kutoka kwenye ghala za AMCOS, udogo wa ghala za AMCOS na uadilifu wa baadhi ya wadau na viongozi kwenye AMCOS.

“Inakuwa ngumu mimi kama ofisa ushirika kujua kama mkulima ameuza zao lake nje ya utaratibu kwa sababu yale yanakuwa makubaliano baina ya mnunuzi na mkulima na pia huyo mnunuzi yule anakwenda kuuza ufuta wake kwenye utaratibu tulioupanga kama serikali wa stakabadhi ghalani.

“Kwetu sisi hakuna kinachopotea kwani takwimu halisi za ufuta uliouzwa, tozo za vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu vinaweza kuonekana baada ya mnunuzi kulipia ufuta wake alionunua mnadani, hivyo kutoka pale tunaamini kila mdau amenufaika na bei iliyopo sokoni.”

Anasema ofisi yake hadi sasa haijapokea kesi, malalamiko wala mashitaka yoyote kuhusu wakulima kudhulumiwa. “Hii inamaanisha wakulima wenyewe wameamua kukubaliana na wanunuzi hao,” anasema kaimu mrajisi huyo.

Hata hivyo, Secilia anasema mwongozo unaosimamiwa na ofisi yake umeweka utaratibu wa kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara na kampuni zinazojihusisha na usafirishaji wa ufuta ambao haujanunuliwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.

KAULI YA SERIKALI

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Ndemanga anasema ili kumaliza changamoto hiyo, upo umuhimu kwa maofisa ugani kutoa elimu kwa wakulima juu ya kujitambua na kulima kibiashara akitambua mfumo mzima wa shughuli zake.

Kuhusu wanunuzi wa ufuta kwa mtindo wa ‘kula maua’, Ndemanga anasema watu hao ni kangomba kama kangomba wengine wanaowarubuni wakulima ambao wananunua mazao nje ya utaratibu na kwamba wanapaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

“Kwa nini umkopeshe pesa alafu umuambie akulipe ufuta? Si akulipe pesa alizokopa, tafsiri hapa unamkopesha shilingi elfu moja na  yeye anakulipa shilingi elfu tatu, maana unampa fedha halafu yeye anakulipa ufuta ambao wewe unakwenda kuuza shilingi elfu tatu. Huko ni kumnyonya mkulima jambo ambalo hatuliruhusu,” anasema Ndemanga.

 

Habari Zifananazo

Back to top button