MOROGORO: SERIKALI kuu imeipatia Halmashauri ya Malinyi, iliyopo mkoani Morogoro gari jipya la kisasa la kubeba wagonjwa (Ambulance) ukiwa ni mpango makakati katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Malinyi , Antipas Mgungusi amesema kuwa, awali aliiomba serikali kuu kupatiwa magari manne ya kubeba wagonjwa kwa ajili ya vituo vya afya Ngoheranga, Itete, Mtimbira, na Hospitali ya Wilaya ya Malinyi.
Mgungusi amesema, kutokana mambo ya bajeti amepatiwa gari moja kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Mbunge huyo, amesema licha ya kupatiwa gari hilo , Wizara ya Afya nayo imeahidi kuwapatia Wananchi wa Malinyi gari jingine la kubebea wagonjwa ndani ya miezi miwili ijayo.
“Ninaimani kuwa gari hili litatumika kwa matumizi sahihi yaliyokusudiwa na mheshimiwa Rais ya kusaidia Wananchi wa Wilaya ya Malinyi katika sekta ya Afya” amesema Mbunge Mgungusi .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi , Rehema Bwasi , baada ya kukabidhiwa kwa gari hilo , ameishukuru Serikali ya awamu ya sita wa kuwapatia gari hilo.
Amesema kuwa gari hilo litasaidia uboreshaji wa huduma za afya kwa wagonjwa na matumizi ya Hospitali ya Wilaya, na kwamba litatunzwa na kutumika kwa matumizi sahihi.
Bwasi ,amesema gari hilo litasaidia kubeba wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya na hivyo kuondoa changamoto iliyokuwepo awali kabla ya ujio wa gari hilo.