Kumenoga Mbogwe, Zahanati saba zafunguliwa
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbogwe imefungua vituo vya afya na Zahanati saba tayari kwa kuanza kutoa huduma wilayani hapo.
Akizungumza katika kituo cha afya Bukandwe leo Oktoba 10, 2023 wakati wa ufunguzi wa vituo hivyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbogwe Dk Jacob Julius ‘Jaju’ amesema vituo hivyo ni kati ya vituo 12 vinavyotarajiwa kufunguliwa kwa mwaka huu ambavyo vitahudumia wananchi 67,596 kwenye kata tofauti tofauti ndani ya Wilaya ya Mbogwe.
Dk Jacob amesema, vituo hivyo ni utekelezaji wa azma ya Rais Samia Suluhu Hassan na serikali ya awamu ya Sita ya kuhakikisha huduma za msingi na za muhimu kwa wananchi zinafika bila kusuasua.
Amesema, katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 serikali imetoa jumla ya Sh Bilioni 1.4 kwa Wilaya ya Mbogwe ikiwa ni fedha za maendeleo ambapo katika fedha hizo, jumla ya Sh Milioni 500 zimeelekezwa katika sekta ya afya.
“Vipaumbele ni kununua vitendea kazi, dawa pamoja na mahitaji ya msingi katika vituo vya afya na zahanati hizi.
”Amesema Dk Jacob
Amesema, mbali na fedha hizo pia, serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada ya afya ambapo kwa mwaka wa fedha ulioisha 2022/2023 watumishi 48 walipangiwa na kupokelewa wilayani Mbogwe.
“Mwaka huu wa fedha 2023/2024 Mbogwe imekwishapokea watumishi 14 na hivyo kufanya jumla ya watumishi 62 ambao wamekwishapokelewa ndani ya mwaka mmoja na miezi miwili.
”Amesema
Aidha, amesema ndani ya muda mfupi, wilaya ya Mbogwe imeweza kutekeleza miradi mikubwa ya kuwahudumia wananchi kwa sekta zote kuanzia afya hadi elimu.
“Hii ni ishara njema na tafsiri kuwa Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan anatujali sana wana Mbogwe na kwa hakika sisi wasaidizi wake pamoja na nyie wananchi hatuna budi kusimamia kikamilifu na kwa uadilifu haya mambo mazuri ambayo yanafanywa na Rais wetu,”amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Jacob, amewataka watumishi wa kada ya afya wilayani humo kuwa na lugha nzuri na zenye staha kwa wagonjwa na kuwakumbusha kuwahudumia watanzania wa Wilaya hiyo kwa usawa bila ubaguzi wa hali wala mali na kwamba hatovumilia mtumishi ambaye atakwenda kinyume na maadili ya kazi.
Naye, diwani wa Kata ya Bukandwe, Joseph Kilonja, amesema kufunguliwa kwa kituo cha afya kwenye kata yake ni jambo ambalo wamelisubiri kwa miaka mingi ambapo ujenzi wake ulianza kwa nguvu za wananchi wenyewe mwaka 2006.
Amesema kwenye kata yake jumla ya wananchi 16,786 kutoka kwenye kaya 1661 watahudumiwa na kituo hicho.