KATAVI: Mkuu wa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, Jamila Yusuf ametembelea na kukagua hatua za mwisho za umaliziaji mradi wa shule maalum ya sekondari ya wasichana Katavi inayojengwa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ili ifikapo Januari 15 shule hiyo ianze kupokea wanafunzi.
DC Jamila akiwa ameambatana na viongozi wa halmashauri hiyo akiwa katika mradi huo, ameridhishwa na baadhi ya hatua zilizofikiwa za kumalizia baadhi ya miundombinu muhimu ikiwemo bweni, vitanda, viti na meza kufikia hatua za mwisho na tayari kwa matumizi ya wanafunzi.
Pamoaja na yote, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nsimbo katika siku chache zilizobaki kusimamia usafi wa viunga vyote vya shule hiyo ikiwemo njia za kupita, maeneo ya viwanja vya michezo pamoja na sehemu ya kujipanga wanafunzi.
Katika hatua nyingine, DC Jamila amesema nyaya za umeme rola 66 zilizobainiwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko kuwa zimeibiwa sasa zimepatikana na wahusika wanaoshukiwa kuziiba wapo katika vyombo vya dola kwa ajili ya hatua zaidi.
Mradi wa Shule maalumu ya Wasichana Katavi unatekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 3 fedha kutoka serikali kuu.