MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imebainisha kuwa bidhaa za tumbaku zina kemikali sumu mbalimbali, zikiwemo zinazosababisha magonjwa ya kansa, huku ikibainisha kemikali zaidi ya 90.
Kutokana na hali hiyo serikali imewekeza mashine za kisasa za kupimia kemikali sumu katika bidhaa zote za tumbaku, ikiwemo sigara.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, kwenye maonesho ya kimataifa ya wadau wa bidhaa za afya ya Afrika Mashariki yaliyoanza jana ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
“TMDA tupo hapa tunashiriki kutoa elimu kama wadau sekta ya madawa na vifaa tiba,” amesema.
“Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, alitembelea banda letu kupata maelezo juu ya kemikali sumu za kwenye tumbaku.
“Kemikali sumu hizi zinasababisha kansa ya damu, kansa ya koo na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza,
“Zikikosekana hizi kwenye bidhaa za tumbaku ndio inapunguza magonjwa kama ya kansa, kubwa zaidi tunataka tuwaoneshe wadau mbalimbali wanaofika kushiriki kwenye maonesho haya,” alieleza Dk Fimbo.
Pia amesema bidhaa zozote za tumbaku, ikiwemo Sigara zinazoingizwa nchini wanazipitia na endapo wakiona zina Kemikali sumu hizo wanaziondoa sokoni.