‘Kuna mabadiliko wanafunzi wa sayansi’

‘Kuna mabadiliko wanafunzi wa sayansi'

Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI, Angellah Kairuki amesema kuwa serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kuanzia shule za sekondari hadi vyuo vikuu.

Waziri Kairuki alisema hayo mjini Kigoma,  wakati akifunga kongamano la wanafunzi wa kike wanaosoma shule za sekondari katika Mikoa ya Kigoma,Tabora na Songwe kujadili changamoto zinazowakabili na kushindwa kufikia malengo na kutafuta njia za kukabili changamoto hizo.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Kigoma, Shukuru Kalegamye, alisema kuwa wanatambua changamoto hiyo hasa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na kubainisha kwamba hali ilivyo sasa ni tofauti na huko nyuma.

Advertisement

Katika kuonesha utekelezaji wa mpango ho alisema kuwa mwaka 2020 wanafunzi wa kike 120,000 walikuwa wamesajiliwa kusoma masomo ya sayansi kwenye mfumo rasmi na usio rasmi nchini na kwamba kufikia mwaka 2022 idadi hiyo ilipanda na kufikia 124,247 na idadi itaongezwa maradufu na taratibu nzuri za kuwafanya wanafunzi hao wafikie malengo yao zinazidi kuboreshwa.

Shukuru Kalegamye Kaimu Katibu Tawala Mkoa Kigoma, ambaye alikwakilisha Waziri wa nchi ofisi ya Raisi TAMISEMI Angellah Kairuki katika kufungua kongamano hilo. (Picha zote na Fadhil Abdallah)

Mmoja wa wanafunzi hao, Dorice Athanas kutoka shule ya Sekondari Malagarasi ya mkoa Kigoma alisema kuwa wanafunzi wengi wa kike wana hamu ya kusoma masomo ya sayansi, lakini  shuleni na nyumbani  kuna maneno ya kukatisha tamaa wanafunzi kwamba masomo hayo ni ya wavulana hivyo wasichana wakisoma hawatafanya vizuri.

Mwanafunzi Aneth Lucas kutoka wilaya ya Urambo mkoani Tabora, alisema kuwa ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi ni changamoto kubwa inayofanya wanafunzi wengi hasa wasichana kukimbia masomo ya sayansi hata kama wanayapenda.

Mwanafunzi mwenye ulemavu wa kusikia kutoka Shule ya Sekondari Kazima Mkoa Tabora, Evodia kimath alisema kuwa wanafunzi wenye ulemavu wana changamoto kubwa katika kusoma masomo ya sayansi kutokana na miundombinu duni ya kujifunza na kufundishia iliyopo, hali inayokatisha tamaa wengi wao kuacha kusoma masomo hayo hasa Kemia,Fizikia na Baiolojia.

Wanafunzi wasichana wa shule za sekondari kutoka mikoa ya Tabora,Songwe na Kigoma wakiwa kwenye kongamano la kujadili changamoto zinazowakabili na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.

Awali Mwakilishi wa TAMISEMI ,Dk Yangson Mgogo ambaye ndiye Mratibu wa mpango wa kuinua kiwango cha wanafunzi wa kike wanaosoma masomo ya sayansi unaotekelezwa kwa pamoja baina ya serikali na Shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) ,alisema kuwa wameanza kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wanafunzi wasichana wanaosoma masomo ya sayansi.