MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango, amesema wananchi wa Tanzania wana manung’uniko mengi ambayo yanaonesha mifumo ya haki jinai ina changamoto kubwa.
Dk Mpango ameyasema hayo leo Januari 31, 2023 mjini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha taasisi za haki jinai.
Amesema:“Katika taifa letu yapo manung’uniko mengi ya wananchi ambayo yanaonesha mfumo wetu wa haki jinai una changamoto nyingi tu, kuanzia ukamataji, wananchi kujua hata haki zao, lakini pia ucheleweshaji wa upelelezi, kwa hiyo malalamiko ni mengi Mheshimiwa Rais.
“Tunapopita huko kukusaidia kazi kwenye mikoa yetu wananchi wanasema mengi, mfano kijana mmoja Mwanza alikamatwa kama mwezi mmoja na nusu uliopita, hakujulikana alipopelekwa, wazazi wake wamejaribu kuhangaika kila mahali ikashindikana, wakienda Polisi hakuna msaada, alihangaika sana.
“Ni wiki iliyopita ndio baba wa kijana amenipa taarifa polisi wamemwambia kijana wapo nae, wakati alishangaika na kutangaza na msiba.
“Kwa hiyo unaona mifumo ambavyo inakuwa na changamoto nyingi, Rais umetumia hekima na busara kubwa ukiwa kama msimamizi wa haki za wananchi, nikupongeze kwa kuunda tume hii,” amesema Dk Mpango.