DODOMA; WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema kumekuwa na wimbi la ongezeko la wanyama katika misitu nchini kutokana na kudhibitiwa kwa uwindaji haramu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo bungeni leo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu, ambapo mbunge huyo alitaka kufahamu mikakati ya serikali kuhakikisha inapitia upya sheria za kulinda hifadhi, ili pia zilinde wananchi.
Katika majibu yake pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu amesema kumekuwa na wimbi la ongezeko la wanyama kwenye misitu kutokana na jitihada za serikali kupitia sheria hizo za udhibiti wa uhifadhi na kulinda uwindaji haramu.
“Lakini pia kumekuwa kumekuwa na wimbi la ongezeko la wanyama kwenye misitu yetu kutokana na jitihada za serikali kupitia sheria zetu hizo za udhibiti wa uhifadhi na kulinda uwindaji haramu.
“Hata hivyo wizara ya maliasili imekuwa ikifanya taratibu kadhaa kukutana na taasisi zinazohusika kwenye uhifadhi wa mazingira yetu na hifadhi za wanyama wetu kuona wanyama wanabaki hifadhini na baadhi ya jitihada zilizochukuliwa ni kuongeza idadi ya askari walioweka vituo kandokando ya hifadhi hizo, kuzuia wanyama wasiingie kwenye makazi ya wananchi, lakini pia jitihada za kufukuza wanyama kwa kutumia ndege kuwarudisha hifadhini,” amesema Waziri Mkuu.