WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa jana ameliaga kundi lingine la wakazi wa Ngorongoro 115 linaloelekea eneo la Msomera lililoko Wilaya ya Handeni mkoani Tanga ambako serikali imeweka miundombinu ya kuwawezesha kuishi katika hali ya utulivu.
Kundi hilo la wakazi 115 lenye kaya 25, linakuwa ni la awamu ya tano ambapo awamu zilizopita zilikuwa ni kaya 106, idadi ya watu ikiwa ni 536.
Pamoja na idadi hiyo kuondoka jana kundi la kaya 1,002 zenye watu 5,382 limejiandikisha mpaka sasa.
Akiwaaga wananchi hao, Waziri Mkuu Majaliwa alisema uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika jambo hilo una nia njema ndio maana amemtuma kutoa neno la faraja kwa wakazi wanaohamia Msomera.
“Ngorongoro hili ni zoezi la pili huku kuna masharti yake chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Kule kuna sheria zake kwani kulima hairuhusiwi, kufanya biashara yoyote hairuhusiwi, kuendesha chombo cha moto hairuhusiwi, kule haturuhusiwi kumiliki ardhi lakini huku mnakoenda mnaruhusiwa,” alisema.
Aliongeza: “Nyie ni Watanzania wenzetu, mmetupa dhamana ya kuwatumikia, tunapaswa tuwe watumishi wenye uaminifu, wenye uadilifu na weledi,” alisema. Aliwapongeza wananchi walioamua kwenda Msomera kwa kuwa uamuzi wao ni mzuri. Kwa maelezo ya Waziri Mkuu, Majaliwa kila kaya inapatiwa ekari 2.5 mpaka tatu katika eneo atakalopewa lenye nyumba yenye vyumba vitatu ikiwa na hati.
“Unaweza kutumia hati hiyo kuombea mikopo. Mmepewa eneo la ekari tano kwa ajili ya malisho kila mmoja. Pia kuna eneo la wazi ambalo mtu yeyote anaweza kulisha mifugo yake,” alisema. Aliwataka wananchi waliobaki Ngorongoro kuiga mfano wa aliyewahi kuwa mbunge wao, Telele kwa kufanya uamuzi wa kuondoka eneo hilo kwa kuwa uamuzi alioufanya sio wa mchezo.
“Majengo yenu mliyoyajenga tunawapa fidia. Leo tunahama kwa hiari tumieni fursa hii. Ninachosema ni kwamba, nia ya serikali ni nzuri na maelekezo ya Rais Samia ni mazuri, tangulieni huko na mimi nitakuja kuwasalimia,” alisema.
Aliwaambia serikali inajua wakitoka katika eneo hilo watakuwa wamefungasha kila kitu hivyo serikali itawapa chakula cha siku ya jana na leo, kisa itawagawia magunia mawili mawili ya mahindi kila baada ya miezi mitatu kwa kipindi cha miezi 18 mpaka msimu wa mvua utakapofika.
Katika hatua nyingine alionya makundi, taasisi na watu binafsi wanaotumika kupotosha kwa kuwahadaa wananchi wa Ngorongoro wasihame. Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana alisema kuwa utaratibu wa kuwahamisha watu hao unakwenda vizuri kwa kuwa wanahamishwa kwa hiari na kwa usalama.
“Tunapenda Ngorongoro ibaki kama eneo la hifadhi.
Niwapongeze wote mlioamua kuhamia Msomera. Mmechagua fungu jema kwa kuwa miundombinu imeshaandaliwa, nyumba ziko tayari,” alisema.