Kuondoa tozo ni uamuzi wa kishujaa
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amemueleza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa uamuzi wa kuondoa tozo na kupunguza baadhi ya tozo katika mitandao ya simu ni uamuzi wa kishujaa.
Nape amesema hayo katika uzinduzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Baharini (Submarine Cable) wa 2 Afrika na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kasi ya 5G ya Airtel leo Agosti 10, 2023 Mbezi Beach Tanki Bovu jijini Dar es Salaam.
“Serikali yako katika kuhakikisha huduma za mawasilino zinamfikia kila mtu kwa bei nafuu na ubora, salama, zenye kubadili maisha ya watu, mwaka huu wa fedha 2023/2024 umefanya uamuzi wa kizalendo na kishujaa kodi ni tozo zilizokuwa zinabebwa na watumiaji wa mawasilino nchini umeziondoa.
“Sio jambo rahisi serikali kuwa na chanzo cha mapato ikakisamehe, ikarudisha kwa wananchi baadhi ya hizo ni kupunguza tozo za miundombinu ya mawasiliano kutoka dola 1,000 hadi dola 200 kwa kuanzia na kutoka dola 1,000 hadi dola 100 kwa kila mwaka ni jambo kubwa,” amesema Nape.
Amesema uwekezaji huo ni mkubwa na kwamba kuna watu wanaziba masikio na kufumba macho kwa kila kitu kinachofanywa na Rais Samia hawakielewi.
“Kwa hiyo Mheshimiwa Rais, hata wale ambao wameziba masikio hawakuelewi tutajaribu kuwaelewesha taratibu watakuelewa, wewe chapa kazi songa mbele, ” amesema.