‘Kuongezeka hati safi ni dalili njema’

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka huu, imeonesha taasisi za serikali zimeboresha uandishi wa taarifa zake za hesabu ndio maana hati safi za ukaguzi zimeongezeka.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh amesema hayo wakati wa mjadala wa wazi kuhusu uwjibikaji na bajeti ya mwaka 2023/24 ulioandaliwa na taasisi ya The Chanzo jijini Dar es Salaam.

Utouh amesema hati safi ya ukaguzi inatolewa kulingana na hesabu za taasisi zilivyotayarishwa kwa kuwa katika ripoti hiyo ikichukuliwa serikali kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma kwa ujumla wao, asilimia 96 wamepata hati safi.

“Hiyo ni dalili njema kwamba nchi baada ya kuamua kufanya kazi zake na kutengeneza hesabu zake kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uhasibu, nchi inakomaa hivyo huo uboreshaji mkubwa wa uandishi wa hesabu,” amesema.

“Ukiangalia ripoti ya CAG mwaka huu na mwaka uliopita,  tumefanya uchunguzi wa ripoti zake tumeona kuwa matumizi yaliyokuwa na viashiria vya rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za serikali yamepungua toka asilimia 13 yaliyoonekana mwaka uliopita hadi kufikia asilimia tisa mwaka huu wa ripoti,” amesema.

Amesema hicho ni kiashiria kizuri hivyo alishauri ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani isiishie tu kwenda kwa Katibu Mkuu Hazina bali ipelekwe kwa Katibu Mkuu Kiongozi ambaye kupitia yeye itafika kwa baraza la mawaziri ambalo Mwenyekiti wake ni Rais.

“Rais na baraza la mawaziri watakuwa na fursa ya kujua utendaji wa serikali kabla ya kutoka kwa ripoti ya CAG,” amesema.

Kwa upande wake Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema endapo bunge likifanya kazi yake zitaonekana faida ya ripoti ya CAG.

“Sasa hivi kuna ma CAG wazuri kuanzia Utoah, Assad na Kichere wanatimiza wajibu wao lakini sio kazi yao kukamata wala kuwajibisha. Kazi yao ni kutoa taarifa tu. Ni wajibu wetu wananchi kuhakikisha baada ya zile taarifa hatua zinachukuliwa na hizo hatua ndizo hizo ama zitachukuliwa kupitia vyombo vya kiuchunguzi au za kibunge,” amesema.

Naye Mhariri Mtendaji wa The Chanzo, Tonny Kirita amesema wamekutana kuangalia masuala muhimu yenye mijadala mipana kwa taifa kwa kuwa tokea Aprili mwaka huu mpaka sasa masuala ya uwajibikaji na ripoti ya CAG yamekuwa yakiripotiwa na vyombo vya habari mbalimbali.

“Lengo ni kujua nini maoni ya wananchi lakini tunajaribu kukutanisha watu pamoja na kuruhusu mjadala kujua watu wanafikiri nini,” amesema.

Aliongeza kuwa lengo ni kuchochea kuwepo kwa mijadala na mawazo ambayo yanajibu maswali kutoka upande wa wananchi.

 

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button