‘Kupikia gesi si anasa, ni lazima’

DAR ES SALAAM: RAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya gesi ya kupikia ni lazima kwa sasa na sio anasa kama ilivyokuwa zamani, lengo ni kuondoa madhara ya kiafya na kimazingira yanayochochewa na matumizi ya nishati chafu ya kupikia kama vile mkaa na kuni.

Rais Samia ameyasema hayo leo Mei 08, 2024 kwenye uzinduzi wa mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia wa Mwaka 2024-2034 uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

“Wengi hawatumii nishati safi kwa sababu ya gharama na uhakika wa upatikanaji. Niwaase sekta binafsi kusogeza huduma zaidi ili iwe rahisi kwa wananchi wa vijijini kupata gesi kwa wepesi,” amesema Rais Samia.

Amesema sababu hizo zinaweza kutatuliwa kwa njia ya ushirikiano miongoni mwa mamlaka mbalimbali za kiserikali na binafsi ikiwemo kutumia teknolojia itakayopelekea upatikanaji rahisi wa gesi kwa bei nafuu.

“Safari yetu ya kimaendeleo haiwezi kupiga hatua ikiwa asilimia 90 ya wenzetu bado wanatumia nishati isiyo rafiki kwa mazingira, nishati na uchumi,” ameasa kiongozi huyo.

Soma pia: https://habarileo.co.tz/gesi-bei-chini-mkaa-juu-chalamila/

Pia, Rais samia amewataka wananchi kubadili fikra ya matumizi ya gesi kwani wanaweza kupika vitu vingi kwa kutumia gesi.

“Kuna imani kuwa ladha ya chakula cha kupikia gesi na mkaa, kuni ni tofauti, hiyo ni Imani tu,” amesema.

Hata hivyo, amewataka Mama Lishe kujikita zaidi katika matumizi ya nishati safi ya kupikia huku akiwaasa wawe na lugha nzuri yenye ushawishi kwa wateja wao wanaotaka matandu katika wali.

Aidha, Rais Samia amewaasa wananchi kudumisha upandaji miti nchini ili kufidia uharibifu uliokwisha fanyika kutokana na shughuli zetu za kila siku ikiwemo ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni na mkaa.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button