Kutokurejesha mikopo, udanganyifu vikwazo mikopo 10%

the close up of the five rows coins ,and the coins jar that fell, with the back ground is a dark blue graph.

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imepewa jukumu la kuhakikisha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vinapata mikopo ya asilimia 10 (4 vijana, 4 wanawake, 2 wenye ulemavu) kwa ajili ya kuendeleza biashara zao na kujiinua kiuchumi.

Tamisemi akiwa msimamizi wa halmashauri za miji, majiji na mikoa, imepewa mamlaka hiyo na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa na kanuni zake zilizotungwa mwaka 2019 chini ya kifungu cha 37 A.

Kifungu cha 4 cha sheria hiyo kinaeleza kuwa mamlaka za serikali za mitaa zina wajibu wa kutenga asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vyanzo vya ndani vya mapato kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Advertisement

Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa, Angelista Kihanga anasema kuwa kwa sasa mfumo wa maombi ya mkopo huo ni kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hivyo kwa kutumia simu janja au kompyuta mpakato, mwanachama anaweza kuingia kwenye mfumo huo.

Kihaga anasema Tanzania ina watumiaji wa simu milioni 43.7 lakini ni milioni 23.1 tu kati yao ndio wanaopata huduma za intaneti.

Anasema asilimia 86 ya wasiopata intaneti wako maeneo ya vijijini ikilinganishwa na asilimia 44.6 waliopo mijini. Pamoja na changamoto hizo anasema serikali kupitia ofisa maendeleo wa kata wamehakikisha vikundi hivyo vinajisajili kwa kutumia mfumo kwa kwenda maeneo yenye mtandao yaliyopo karibu na maeneo wanayoishi.

“Kabla ya mfumo huu vikundi vilikuwa vinapeleka maombi yao kwenye halmashauri kwa mkono. Takwimu zinaonesha kabla ya mfumo utekelezaji ulikuwa ukikumbwa na changamoto kadhaa ambazo zimeondolewa baada ya kuanza mfumo,” anasema Kihaga.

Anaongeza kuwa miongoni mwa changamoto zilizokuwepo kabla ya mfumo huo ni uwepo wa vikundi hewa, kukosekana uwiano wa mgawanyo wa asilimia za mikopo kwa vikundi na walengwa na watu kujiandikisha zaidi ya kikundi kimoja.

Pia anasema changamoto nyingine ni ya marejesho, kukosekana kwa mikakati madhubuti ya kusimamia urejeshaji wa mikopo, utata wa usajili wa vikundi na kuwepo kwa vikundi ambavyo namba zake zimejirudia zaidi ya kikundi kimoja.

Kihaga anasema kukosekana kwa uwazi kwenye kutoa mikopo kulichangia kuanza kwa mfumo huo.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, Mkurugenzi kwa mamlaka yake kama Ofisa Masuuli amepewa wajibu wa kuhakikisha kuwa inatenga mikopo hiyo na kutolewa kwa kuzingatia kanuni hizo ambazo vikundi vilivyokopeshwa vinarejesha mikopo kwa wakati.

Pia anapaswa kuzingatia mgao wa fedha za mikopo kwa kugawa asilimia 40 ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, asilimia 40 kwa ajili ya vijana na asilimia 20 kwa vikundi vya watu wenye ulemavu bila kutoza riba.

Kanuni hizo pia zinaeleza sifa za vikundi kupata mkopo kama vile kusajiliwa, kujishughulisha na ujasiriamali au kinakusudia kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati.

Masharti mengine ni kila kikundi kuwa na akaunti ya benki iliyofunguliwa kwa jina la kikundi hicho na kwa ajili ya matumizi ya kikundi na kipaumbele ni kwa raia wa Tanzania wenye akili timamu.

“Ofisi ya Rais Tamisemi ndio inayosimamia upatikanaji na utengenezaji wa mfumo huu, miundombinu yetu inatumia jenereta na umeme wa jua kama vyanzo vingine vya kuzalisha nishati ya umeme lakini pia tuna seva mbili kwa ajili ya kuhakikisha kwamba moja ikiwa na hitilafu nyingine itatumika kwa ajili ya kuhakikisha huduma endelevu za mikopo zinapatikana.”

Anafafanua kuwa hatua za mwanachama au kikundi kusajili kupata mkopo kwa njia ya mfumo huo ni kufungua akaunti itakayomuwezesha kuingia kwenye mfumo na kwamba kiongozi wa kikundi ndiye anapewa jukumu la kuhariri taarifa za kikundi.

Kikundi kinaweza kusajili jina la kikundi na kupewa cheti ambacho watakipeleka benki kwa ajili ya kufungua akaunti na usajili wa wanachama unalenga kuwatambua ili anapofungua na kikundi kingine asiweze kukubaliwa mpaka pale ambapo atatolewa kwenye mfumo huo.

Ili kikundi kisajiliwe wanatakiwa kutimiza idadi ya wanachama ambapo kwa vikundi vya wanawake na vijana ni kuanzia watu watano na kuendelea na vijana hawatakiwi kuzidi umri wa miaka 35.

Mkurugenzi huyo anasema mfumo huo umesaidia kuimarika kwa usimamizi na ufuatiliaji wa marejesho na shughuli za vikundi kwa sababu ni rahisi kuwapata wanachama wote wa kikundi kupitia vitambulisho vya taifa (NIDA) ambavyo hutumika wakati wa usajili (mfumo unabadilishana taarifa na NIDA).

Vilevile anasema mfumo huo umeunganishwa na Wakala wa Serikali Mtandao (GePG) hivyo marejesho yote yanafanyika kupitia nambari ya udhibiti ambayo kikundi kinaweza kulipa kwa kutumia mitandao ya simu, mawakala wa benki na benki.

“Vikundi vinauwezo wa kujua hali ya marejesho ya mikopo yao kupitia mfumo huu kwa kuwa kuna moduli ya ufuatiliaji inayomuwezesha ofisa maendeleo ya jamii kupata taarifa za kikundi kwa urahisi kwa sababu mfumo una taarifa za vikundi na idadi ya vikundi vinapopatikana nchini,” anafafanua.

Kuhusu utoaji wa elimu, Kihanga anasema wanaendelea kutoa elimu kuanzia kwa wakufunzi ngazi ya mkoa na halmashauri na wao huenda kutoa mafunzo katika ngazi ya kata na maofisa maendeleo ngazi ya kata hutoa mafunzo kwenye vikundi.

Anasema sababu zitakazochangia kikundi kupoteza sifa ya kupata mkopo ni kutomaliza kurejesha mkopo uliotolewa, kutoa taarifa za uongo kwa mamlaka hizo kwa lengo la kupata mkopo na kutumia fedha za mkopo kwa matumizi tofauti na yale yaliyoombewa mkopo bila ya idhini ya mamlaka ya serikali ya mtaa au kushindwa kurejesha mkopo kabisa.

Kanuni hizo pia zinatoa adhabu kwa mtu atakayetumia fedha hizo kwa matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Kamati ya Kudumu ya Fedha, Mipango na Uongozi na atakayetoa taarifa za uongo kwa lengo la kujipatia mkopo unaotolewa chini ya kanuni hizo.

“Mpaka sasa tumetoa zaidi ya Sh bilioni 100 kwa vikundi vya halmashauri tangu kuanza kwa huduma hii mwaka 2018/19 lakini niwakumbushe kuwa mwanachama atakuwa ametenda kosa na endapo atatiwa hatiani atatozwa faini ya kiasi kisichopungua Sh 200,000 na kisichozidi Sh milioni moja au kutumikia kifungo kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miaka miwili,” anasema.

Kihaga anasema Tamisemi imekuwa ikishirikiana na mradi wa kuimarisha mifumo ya sekta za umma unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID PS3+) kuboresha mipango na bajeti katika halmashauri ili ziweze kuzingatia vipaumbele vya wananchi.

Mradi huo umekuwa ukiwasaidia halmashauri kutoa kipaumbele kwa radio za jamii ili ziwefikie wananchi hususani wanawake, vijana na wenye ulemavu kuhusu mikopo na wajibu wao kutumia na kurudisha kwani hizo ni fedha za umma.

“PS3+ imeboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha za umma katika ngazi za halmashauri, vijiji na mitaa, kata na vituo vya kutolea huduma. Mifumo hii inazisaidia halmashauri kuboresha ukusanyaji wa fedha na pia kusimamia fedha zao na hivyo kuweza kufikia malengo yao ya kutoa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa sheria na kanuni,” anasisitiza.

Kupitia mifumo iliyoboreshwa na mradi huo mapato yote ya halmashauri kutokea vituo vya afya, vijiji au mitaa na kata yanaingia kwenye mifumo ili yatumike vizuri katika kutoa huduma ikijumlisha mikopo ya halmashauri ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mradi wa PS3+ umeboresha mifumo ya kuwapatia mafunzo ya majukumu yao watendaji kata, vijiji na mitaa waweze kutoa huduma bora kwa wananchi ikijumlisha kuwahamasisha wanawake, vijana na wenye ulemavu kuhusu mikopo ya asilimia 10.

1 comments

Comments are closed.