DODOMA; SERIKALI imesema gharama ya Sh 177,000 kuunganisha umeme vijijini kwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ilifutwa na sasa ni Sh 27,000.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ametoa kauli hiyo bungeni leo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahya Massare aliyetaka kujua ni lini serikali itarejesha gharama za kuungaishiwa umeme kuwa Sh 177,000.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kapinga amesema: “Kulingana na bei za umeme zilizopitishwa na EWURA, gharama za kuunganisha umeme wa njia moja katika maeneo ya vijijini ni Sh 27,000 na mijini Sh 320,960. Kwa kipindi cha nyuma, kwa miradi ya vijijini, REA ilikua inatoza Sh 27,000 na TANESCO Sh 177,000.
“Kutokana na malalamiko ya wananchi ya utofauti wa bei kati ya REA na TANESCO ya kuunganisha umeme vijijini, Serikali iliamuru TANESCO kushusha bei ya kuunganisha umeme vijijini na kuwa Sh 27,000 kama REA na tofauti ililipwa na Serikali kama ruzuku kwa TANESCO.
“Kwa hali hiyo, bei ya Sh 177,000 iliyokuwa inatozwa na TANESCO vijijini ilifutwa na kuwa Sh 27,000 kwa vijijini kama ilivyo sasa,” amesema Naibu Waziri Kapinga.