KUWASA yatangaza operesheni wezi wa maji

KIGOMA: Mamlaka ya maji safi na maji taka Kigoma Ujiji imetangaza kuendesha operesheni maalum ya kukamata watu wanaojiunganishia maji bila kufuata taratibu jambo linaloitia hasara mamlaka hiyo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Poas Kilangi akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma amesema  mpango huo unakuja kufuatia ziara aliyofanya ambayo amegundua kuwepo kwa wizi na uchepushaji maji unaofanywa katika maeneo mbalimbali mtaani kwenye manispaa ya Kigoma Ujiji.

Kutokana na hali hiyo Mkurugenzi huyo ametoa wiki mbili kwa watu wote wanaotumia maji bila kufuata taratibu (wezi) kujisalimisha kwa uongozi wa mamlaka hiyo kwani baada ya muda huo mamlaka itachukua hatua za kisheria kwa watu wote watakaobainika kufanya kosa hilo.
Katika hatua nyingine Kilangi amewataka wateja wanaotumia maji yanayozalishwa na mamlaka hiyo hasa nyumba za ibada, masoko na mitaani kutumia maji hayo vizuri kuepuka matumizi makubwa yasiyo na tija ambayo yanawafanya kulipa bili kubwa.

Advertisement

Akizungumzia operesheni hiyo ya KUWASA Mratibu wa Shirika la Nyakitonto Youth Development, Ramadhani Joel amesema shirika lake kwa kushirikiana na KUWASA liliendesha mradi wa uwajibikaji kwa watendaji wa mamlaka hiyo kusikiliza kero za wananchi na upande wao wananchi kushirikiana na mamlaka kusaidia mivujo na  wizi wa maji.

Hata hivyo amesema kuwa licha ya mafanikio ya mradi huo ambao uliwajengea uwezo wananchi kutoa taarifa za mivujo na wizi bado baadhi ya watendaji wa mamlaka hiyo siyo waaminifu na ndiyo kwa kiasi kikubwa wanashiriki kwenye mpango wa kuwaunganisha watu maji bila kufuata taratibu na kusababisha wizi wa maji na kumuomba Mkurugenzi huyo kuwabaini watendaji hao na kuwachukulia hatua.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *