‘Kuwe na jukwaa moja watekelezaji haki jinai’

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amependekeza ushirikiano, ushirikishwaji wa jukwaa moja litakalohusisha watekelezaji wa majukumu ya haki jinai, ili kuweza kupeana taarifa muhimu zinazohusu haki jinai.

Pia amependekeza makosa ya jinai kuwekwa kwenye sheria moja ya kanuni ya adhabu sura ya 16 pamoja na kwenda kufanya utafiti kwenye makosa ya uhujumu uchumi, ili kulinda uchumi wa taifa.

Amesema hayo Dar es Salaam leo,  alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha mapendekezo kwa Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini.

Ndumbaro alisema Wizara ya Katiba na Sheria, ndio wizara yenye majukumu ya kusimamia mfumo mzima wa haki jinai na ina taasisi nyingi zilizopo chini yake na ndio inajua kiatu cha sheria wapi kinabana, ndio maana wameangalia miundo na mifumo ya haki jinai ikiwemo sheria katika maeneo mbalimbali.

“Tunahitaji kuwa na jukwaa la pamoja ambalo litahusisha wote wanaotekeleza majukumu ya haki jinai, ili waweze kuwa kwenye jukwaa moja na kubadilishana taarifa mbalimbali zinazohusu haki jinai,” alisema  Dk Ndumbaro na kuongeza kuwa:

“Ilivyo sasa kila taasisi inafanya kazi kwenye kiota chake, ndio maana  tumependekeza mbele ya tume hii kwamba pamoja kuendelea kuwa na hivi viota vyetu, lakini tuwe na mfumo wa kubadilisha taarifa zinazohusiana na haki jinai.”

Pia alisema wamependekeza waangalie sheria ya makosa ya jinai, sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 ili ikiwezekana makosa yote ya jinai yawe ndani ya sheria hiyo.

“Makosa hayo yote yakiwa kwenye sheria moja itasaidia hata kwa mwananchi kuweza kuju,  lakini itasaidia hata kwenye vyombo vya utekelezaji kuweza kutekeleza kwa ufanisi zaidi, itasaidia hata kwenye mhimili wa mahakama kutoa tafsiri stahiki inayopaswa kuzingatiwa,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button