Kwa haya, hongera Kamati ya Kudumu ya Bunge
NAMSHUKURU Mungu na uongozi wa gazeti la HabariLEO kupata nafasi ya kuipongeza kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Pongezi hizi zinatokana na juhudi inazofanya kuhakikisha sekta inazozisimamia zinatekeleza majukumu yake kwa uhakika na ufanisi mkubwa.
Kilichonisukuma kutoa pongezi hizi ni hatua ya Kamati kukutana na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Tafiti za Misitu na Nyuki nchini (Tanzania Forestry Research Institute–TAFORI).
Nikiwa Mwenyekiti wa bodi ya 11 ya Tafori ambayo muda wa kuisimamia taasisi hiyo ulimalizika Novemba 7, mwaka huu (2022), nimeona ni vyema niungane na wajumbe wa kamati hii kumpa nafasi Mtendaji Mkuu wa Tafori, Dk Revocatus Mushumbusi kutoa maelezo na ufafanuzi kuhusu nini taasisi inatakiwa kufanya na inafanya hadi sasa.
Ni jambo jema pia lililofanyika kuiwezesha kamati hiyo kukutana na kujadili masuala muhimu kuhusu tafiti za misitu na ufugaji nyuki nchini kwa maslahi mapana ya taifa.
Majukumu ya Tafori ni kufanya tafiti kuhusu rasilimali misitu na ufugaji nyuki nchini. Ilianzishwa mwaka 1980 kupitia Sheria Namba 5, Sura ya 277 na sasa ni miaka 42 imetimia. Wakati wote huo taasisi hiyo imekuwa ikifanya tafiti kulingana na mipango ya muda mfupi na muda mrefu.
Hata hivyo, changamoto kubwa ambayo naweza kuita kisababishi kikubwa kwa Tafori kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo, ni ufinyu wa bajeti na uhaba wa wataalamu muhimu wanaotakiwa. Najua serikali inafanyia kazi hili kuhakikisha inasonga mbele na kuhakikisha matumizi ya rasilimali misitu na ufugaji nyuki ni endelevu na kwa faida ya vizazi vyote.
Kwa kiasi kikubwa, utekelezaji wa majukumu ya Tafori kupitia tafiti mbalimbali, umekuwa ukiwezeshwa na wahisani zaidi kuliko fedha zinazotolewa na serikali.
Kwa miaka ya nyuma hali ya Tafori ilikuwa nzuri hasa wakati wa msaada kutoka Serikali ya Ufini (Finland) kupitia mradi wa tafiti za misitu nchini (Forest Research Support in Tanzania-FORST). Msaada uliotolewa na wahisani ulikuwa takribani Sh bilioni 2.6 (kwa viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni kwa wakati huo).
Baada ya mradi huo kuanza Julai, 1996 na kumalizika robo ya kwanza mwaka 2002 na wahisani kusitisha msaada waliokuwa wanautoa, hali ya Tafori haikuwa ya kutia moyo. Shughuli za uendeshaji za kawaida zilizogharimu Sh bilioni 46 kwa mwezi (Sh bilioni 552 kwa mwaka) ikawa changamoto hasa utafiti.
Nilipopata taarifa kwamba Mtendaji Mkuu wa Tafori, Oktoba 26, mwaka huu (2022) alikutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na kuieleza Tafori nini inatakiwa kufanya kisheria na nini changamoto wanazokumbana nazo, jitihada uongozi wa taasisi ulizofanya kutatua changamoto, hakika nilisema Mungu mkubwa kwa kutambua kwamba ni nafasi adimu ambayo Tafori imewahi kupata.
Kwa utumishi wangu wa miaka 35 kuanzia mwaka 1977 mpaka Desemba 12, 2012 nilipostaafu, sikuwahi kusikia Bunge kupitia kamati zake imechukua hatua kama hiyo. Naweza kuwa nimesahau lakini Menejimenti ya Wizara tulikuwa tukikutana na Kamati za Kudumu za Bunge na kuongelea masuala mbalimbali kuhusu usimamizi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizohusu rasilimali misitu na ufugaji nyuki ikiwemo masuala ya kufanya tafiti lakini sikuwahi kusikia Mtendaji Mkuu wa Tafori amepewa fursa ya kukutana na kutoa maelezo kama ilivyofanyika Oktoba 26, mwaka huu katika moja ya kumbi za Bunge jijini Dodoma.
Kuna nyakati wajumbe wa kamati za kudumu na hasa iliyokuwa ikihusika na shughuli za maliasili na utalii, wamekuwa wakitembelea na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Tafori makao makuu Morogoro. Hata hivyo, kitendo cha Kamati ya Kudumu ya Bunge la sasa kumpatia fursa Mtendaji Mkuu wa Tafori, kukaa naye Dodoma kwa nia ya kuielewa Tafori katika uhalisia wake na mchango wake kwa maendeleo ya misitu na ufugaji nyuki nchini na kwa maslahi mapana ya Watanzania wote, ni uwajibikaji wa kupongeza.
Ni kupitia kamati hiyo, Bunge litaweza kuyafahamu matatizo yanayoikabili taasisi hiyo, ufinyu wa bajeti na kuyatafutia ufumbuzi wa haraka.
Wajumbe wa kamati hiyo ambao ni wabunge kupitia majimbo mbalimbali nchini baada ya kupokea taarifa kuhusu Tafori, walishituka kuona taasisi muhimu kama hiyo haina fedha za kutosha kuiwezesha kumudu majukumu yake ya kisheria na badala yake baadhi ya watafiti wamekuwa wakihangaika kuomba fedha za kufanya tafiti kwa kuandika miradi inayoendana na mahitaji ya mtoa fedha.
Upatikanaji fedha za kufanya tafiti kwa njia hii ya kutoka kwa wahisani nje ya nchi kunafanya tafiti zisiendane na mahitaji halisi.
Pamoja na Tafori kunufaika na fedha za wahisani, pia Mfuko wa Misitu Tanzania (Tanzania Forest Fund-TaFF) umekuwa nyenzo muhimu kwa kuisaidia taasisi hiyo kutoa ruzuku kwa baadhi ya watafiti kutekeleza miradi ya tafiti za misitu na ufugaji nyuki.
Hii ni pamoja na kuiwezesha Tafori kutimiza baadhi ya majukumu yake kwa kuipatia mtambo ya kupima ubora wa mbao ili kubaini matumizi yake, vifaa vya kupima matumizi ya maji kwa aina mbalimbali za miti.
Vilevile, TaFF imeisaidia taasisi kwa kuipatia magari mapya mawili ambayo yamekuwa tegemeo kubwa kwa shughuli za utawala na kufanya tafiti nje ya makao makuu, Morogoro.
Namshukuru Katibu wa TaFF, Dk Tuli Msuya na watendaji wote wa mfuko huo bila kuisahau bodi ya mfuko huo kwa kuiwezesha Tafori kutoa mchango zaidi kwa lengo la kupata matokeo chanya na maendeleo yenye tija katika misitu na ufugaji nyuki.
Makala ijayo itaeleza zaidi kuhusu mchango wa TaFF kwa Tafori na kilichojiri katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge na Mtendaji Mkuu wa Tafori, matarajio yangu kwa Tafori kufanya vizuri zaidi baadaye kuliko hali ilivyo sasa.
Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki mstaafu.