RAIS wa zamani wa USSR, Mshindi wa tuzo ya Nobel, Mikhail Gorbachev aliaga dunia Agosti 30 mwaka huu, akiwa na umri wa Miaka 91. Marehemu Gorbachev anabaki katika historia ya kumalizika kwa Vita Baridi na kusambaratika kwa USSR.
Wakati mwanasiasa Mikhail Gorbachev hatunae tena dunia, nimelazimika kurejea tena kusoma waraka wa mtaalam katika Sayansi ya Siasa, Francis Fukuyama, alipoandika waraka wenye kichwa cha maneno: “The End of History”, akielezea mvutano wa kiitikadi ya Ubepari na Ukomunisti kuwa sasa vita hivyo vimefikia ukingoni kwa ubepari kushika kasi na ukomunisti kudhoofika zaidi na kutoweka.
Kwa mara ya kwanza waraka wake, Francis Fukuyama, ulichapishwa katika jarida la Marekani mwaka 1989, akielezea kuanguka kwa itikadi ya Ukomunisti katika Ulaya Mashariki na sehemu nyengine ya Dunia.
Marehemu Gorbachev alijitahidi kunusuru Ukomunisti usianguke, kwa kuanza kuchukua hatua mbalimbali za mageuzi ya kiuchumi kwa kuchukua mambo mazuri ya itikadi Ubepari kuchanganya na Ukomunisti, ili waendelee kubakia katika itikadi yao, lakini hakuweza kuungwa mkono na makada wa chama cha Kikomunisti.
Gorbachev hakutafuna maneno katika kutetea masimamo wake wa mageuzi ya kiuchumi, aliwaambia mambo mawili ambayo alidhani yatakuwa kinga ya kuzuia Ukomunisti usishindwe katika USSR.
Akihutubia Mkutano Mkuu wa 27 wa Chama cha Kikomunisti mwaka 1986, Gorbachev aliwaambia wajumbe wa chama chake kwamba lazima sasa wakubali kile alichokiita “Perestroika”, akiwa na maana ya mpango wa mageuzi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Gorbachev akawatajia jambo jengine la pili katika kuokoa Ukomunisti usisambaratike ni “Grasnost”, akiwa na maana ya sera itakayofungua milango ya uwazi katika jamii, kuruhusu mijadala na uhuru wa maoni kwa raia.
Mambo yalizidi kuwa magumu kwa Gorbachev, kelele za mageuzi ya kiuchumi na kisiasa yalizidi kushika kasi kila kona ya USSR, Yugoslavia, Czechoslovak, Romania wananchi hawasikii lolote zaidi ya kutaka mageuzi ya kiitikadi.
Katika mkutano muhimu wa kilele uliofanyika Visiwa vya Malta katika Mji Mkuu wa nchi hiyo, Valetta Desemba 2 mwaka 1989, baina ya Marekani na Urusi, viongozi wa nchi hizo, Rais George H.W. Bush na Mikhail Gorbachev walikubaliana kuunga mkono mageuzi ya kiitikadi, huku Gorbachev akichukuwa maamuzi magumu yaliyogharimu uongozi wake.
Chombo cha kuzama hakina usukani, Dola kubwa lenye nguvu za kijeshi na kiuchumi, “Union of Soviet Socialist Republics”(USSR) likasambaratika na kuzaliwa nchi 15.
Nchi hizo mpya ni Armenia, Azerbaijan, Belarus, Estonia, Georgia, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Latvia, Lithuania, Moldova, Russia, Tajikistan, Turkmenistan, Ukraine na Uzbekistan.
Upepo ule haukuishia kwa USSR,bali iliyokuwa Muungano wa Yugoslavia nao ukajikuta katika kile kilichotokea USSR.
Leo hakuna tena “Socialist Federal Republic of Yugoslavia” na badala yake kuna Slovenia, Macedonia, Croatia, Serbia, Montenegro na Bosnia.
Pia “Czechoslovak federation” haikuweza kuhimili vishindo,kama ilivyo kwa USSR,Yugoslavia Shirikisho hili nalo likasambaratika na kila mmoja kubaki na nchi yake, nchi mbili zikapatikana “Czech Republic na Slovakia”
Tukirudi katika mkutano uliofanyika Malta mwaka 1989, msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje wa USSR, Gerasimov alitangaza kwamba “I think the brezhnev doctrine is dead” kwa tafsiri isiyokuwa rasmi ni kwamba: “Ninafikiri nadharia ya Brezhnev imekufa.”
Hakuishia hapo akaendelea kusema “superpower had “buried the cold war at the bottom of the Mediterranean sea,” Mataifa makubwa yamezika vita baridi chini ya bahari ya Mediterrania.
Wakati mkutano katika Visiwa vya Malta ulifanyika, katika Mwezi wa Novemba mwaka 1989 Serikali ya Ujerumani ya Mashariki kwa wakati huo majira ya saa 1:00 usiku ilitangaza kwamba mpaka unaotenganisha Ujerumani Mashariki na Magharibi utakuwa wazi!
Tangazo hili liliashiria zama mpya, kuanguka kwa ukuta wa Berlin ,kumalizika kwa vita baridi na kupungua nguvu kwa itikadi ya ukomunisti na kuimarika kwa itikadi ya Ubepari na Mataifa ya Magharibi kuanza kusherehekea ushindi
Tukirudi katika mkutano wa kilele, kule Malta, Rais Bush na Gorbachev kwa pamoja wakakubaliana kuwa hakuna tena vita baridi, kilichopo ni suala zima la kukuza uchumi katika nadharia mpya kulingana na matakwa ya ulimwengu wa sasa unavyotaka.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Gorbachev alisema: ”We searched for the answer to the question of where do we stand now,” Mr. Gorbachev, ”We stated, both of us, that the world leaves one epoch of cold war and enters another epoch.”
Kwa matamshi haya ya Kiongozi huyo wa USSR, Taifa kubwa lenye nguvu, Marekani na washirika wake wa upande wa Magharibi walifanikiwa kuvizika vita baridi na Ukomunisti katika upwa wa bahari ya Mediterrania.
Mashabiki wa itikadi ya Ubepari kama Francis Fukuyama na wengine, wakaanza kusherehekea kifo cha Ukomunisti na tangu wakati huo mfumo wa Uliberali ulizidi kushamiri katika mataifa mbalimbali.
Ikumbukwe kwamba kusambaratika kwa USSR, hakukuwa na maana nyingine zaidi ya kuashiria kuanguka kwa itikadi ya Ukomunisti, ingawa dola kubwa lilianguka, lakini kuanguka huko kulifurahiwa na wengi.
Kuzuka kwa vita baridi kulitokana na kumalizika kwa vita vya pili vya dunia mwaka 1945 kulikosababishwa na mashabiki wa itikadi mbili ile ya Ukomunisti wakifuata mafundisho ya kina Karl Marx, Frederick Engels, Vladimir Lenin na wengineo.
Mashabiki wa Itikadi ya Ubepari wakifuata mafundisho ya Adam Smith, David Ricardo, John Stuart Mill, Jean-Baptiste Say, John Maynard Keynes, Milton Friedman, Friedrich Hayek. Mvutano wa nadharia mbili hizo kukazaa kambi mbili zenye kuvutana kuhusu uchumi na utawala.
Kwaheri Mikhail Gorbachev.