Kweleakwelea waharibu mashamba ya wakulima

TAKRIBANI heka 1,600 za mashamba ya mpunga Kata ya Kagu, Halmashauri ya Wilaya ya Geita mkoani hapa, zipo hatarini kushambuliwa na ndege aina ya kweleakwelea.

Ofisa Kilimo wa Halmashauri, Malick Athuman alitoa taarifa hiyo juzi katika mahojiano maalumu na HabariLEO akisema tayari mawasiliano na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatirifu (TPHPA) yamefanyika, ili kuwadhibiti ndege hao ambao idadi yao inaonekana kuongezeka katika eneo hilo.

“Tulifanya hivyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa vijiji vya Kagu na Isima, kwamba tayari ndege wamevamia mashamba na kufanya uharibifu wa zao hilo. “Maofisa wa mamlaka husika wako njiani wanakuja. Hata msimu uliopita tulipata tatizo hili katika Kijiji cha Isima, tukalitatua kwa njia hii, ndege wote wakaisha,” alisema.

Aliwahakikishia wakulima kwamba changamoto hiyo itaisha, kwa uendelevu wa zao hilo la chakula na biashara. Pamoja na kuwathibiti kweleakwelea shambani, mamlaka itapulizia dawa kwenye mazalia yao kwa kutumia helikopta, ili kuangamiza kabisa chimbuko lao, alisema.

“Kawaida ndege hawa huvutiwa na mazao mengi, ikiwemo alizeti, lakini tumegundua wanapendelea zaidi mpunga kiasi kwamba wanaweza kuhama haraka kutoka shamba moja kufuata jingine,” alibainisha na kusistiza: “Kuwadhibiti ni lazima kwa sababu wanafanya uharibifu mkubwa kwa kuanza kushambulia mmea wenyewe, hadi pale mpunga unapoelekea kukomaa”.

Ilifahamika zaidi kwamba kweleakwelea wana uwezo wa kuharibu shamba zima kwa silimia 100, kiasi cha mkulima kutopata hata punje ya mavuno.

Habari Zifananazo

Back to top button