Kyerwa roho kwatu changamoto ya tembo kutatuliwa

KAGERA;Kyerwa. Wananchi wa vijiji vitano katika Kata ya Businde, Wilaya ya Kyerwa, wameipongeza serikali kupitia uongozi wa hifadhi za Taifa za Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagawe, kwa kutatua changamoto ya kukabiliana na wanyama wakali kama tembo waliowakimbiza katika makazi yao na kuacha shughuli za uzalishaji kwa kipindi cha miaka 10.

Wananchi wakiambatana na wenyeviti wao walifanya mkutano wa hadhara na kuwasilisha pongezi zao mbele ya makamishina wasaidizi wa uhifadhi kutoka hifadhi hizo na Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Zaituni Msofe.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibale Erasto Waziri, akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa vijiji vya Kibale, Nyakashenye, Kijumbula, Businde na Bugala, amesema walikuwa katika mazingira magumu ya kupambana na wanyama hao, hivyo kuyatelekeza mashamba yao kuepuka vifo na majeraha.

Amesema karibu miaka 10 wamekuwa hawavuni mazao vizuri, lakini sasa wanashukuru watavuna mazao na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kama kawaida.

Amesema wakuu wa hifadhi hizo walitumia taaluma zao kuondoa kero ya tembo kwa muda mfupi na kumshukuru Mkuu wa Wilaya kwa usimamizi wa jambo hilo.

Ameeleza kuwa hakuna changamoto isiyo na mwisho, kwani awali walifikia hata kujenga shule shikizi kutokana na changamoto hiyo ya wanyama.

Mkuu wa hifadhi ya Ibanda Kyerwa,  Dk Fredrick Mofulu, amesema alihamia katika hifadhi hiyo mwaka 2022 na changamoto kubwa aliyokutana nayo ilikuwa ni kero ya wanyama hao kuvamia maeneo ya wananchi na kusababisha madhara makubwa.

Amesema Novemba 11,mwaka huu waliweka kambi katika kitongoji cha Maendeleo Kijiji cha Nyakashenye wilayani humo, ambacho nusu ya wanakitongoji walikimbia makazi yao na kufanya tathimini ya hao tembo na jinsi ya kuwaondoa.

“Taaluma niliyoisomea ni mnyama tembo namfahamu vizuri kwa kumsoma kwa maandishi na kwa kuishi naye, hivyo nilichogundua baada ya zoezi hili tunaweza kuondoa changamoto ya tembo katika maeneo yote,“amesema Dk Mofulu na kuongeza kuwa waliondoa tembo hao kwa muda wa siku nne kwa mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano wa wananchi.

Naye Mkuu wa Wilaya Msofe, amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku na kuwahakikishia waliohama maeneo yao kurudi katika vijiji vyao na kupongeza viongozi wa uhigfadhi kwa kazi yao ya kuondoa wanyama hao.

 

Habari Zifananazo

Back to top button