Kyerwa watakiwa kutunza miradi ya maji

WANANCHI wa Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera wametakiwa kutunza miradi ya maji ili idumu.

Kauli hiyo imetolewa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022, Sahili Geraruma, wakati akiweka  akiweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Kagenyi, Omukalinzi, wenye thamani ya Sh milioni 260, utakaowasaidia wananchi zaidi ya 3,000  katika Kijiji cha  Kagenyi, Kyerwa.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inahakikisha mamlaka ya  maji  zinatekeleza majukumu yake ya kumtua ndoo mama kichwani  na kuhakikisha kuwa, idadi ya wananchi wa vijijini wanaopata maji safi na salama inaongezeka.

Alisema ili kuunga mkono juhudi za serikali, ni vizuri wananchi wakaitunza miradi hiyo na kuilinda, ikiwemo kutohujumu miradi, kuhakikisha wanaunganisha maji nyumbani, kulipa bili na kutoa taarifa kwa wakati katika mamlaka za maji pale wanapoona miradi inahujumiwa.

“Niwapongeze RUWASA mkoani Kagera, naona kila mradi tunaopitia unatekelezwa kwa viwango sana, hii inaonesha mnajituma, naomba kwa nafasi yenu mhakikishe wananchi wanapata maji safi na salama.

“Kwa moyo wa dhati naweza kusema kuwa chombo hiki kimefuta historia kuwa ya vijiji, ambavyo havikuwa na maji tangu Uhuru,” alisema Geraruma.

Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Inocenti Bilakwate, alisema kuwa uwepo wa mradi wa maji wa Kagenyi, utasaidia wananchi wanaotembea zaidi ya kilometa 8 hadi 10, kufuata maji katika madimbwi yasiyo salama, ambayo yanatumiwa na mifugo na binadamu.

Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa Kyerwa, Shukuran Tundaraza,  alisema mradi ulianzishwa  mwaka 2021, lengo likiwa ni kusaidia wananchi kupata maji safi na salama,  lakini kuwezesha  Hospital ya Wilaya ya Kyerwa kupata maji na unatarajiwa kukamilika Oktoba 30 mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button