TAKWIMU zinaonesha laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka milioni 55.7 mwezi Aprili, 2022 hadi kufikia milioni 62.3 mwezi Aprili, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 11.8.
Sambamba na hilo watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka milioni 29.9 mwezi Aprili, 2022 hadi kufikia Milioni 33.1 mwezi Aprili, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 10.7.
Takwimu hizo zimetolewa na Waziri Nape Nnauye wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na teknolojia ya habari kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Katika taarifa yake ya bajeti, Waziri Nape amesema vituo vya kurusha matangazo ya redio vimeongezeka kutoka 210 mwaka 2022 hadi kufikia vituo 215 mwezi Aprili, 2023 na vituo vya kurusha matangazo ya runinga vimeongezeka kutoka 56 mwaka 2022 na kufikia vituo 65 mwezi Aprili, 2023.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya matumizi ya teknolojia za utangazaji hasa maudhui mtandaoni ambayo pia yamechangia kuongeza ajira kwa vijana. “Takwimu hizi zinaashiria hali ya ukuaji wa Sekta.’ Amesema Nape