Laini za zimu zafikia milioni 58 Tanzania

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema kuna ongezeko la asilimia 3.4 ya laini za simu, huku matumizi ya huduma za intaneti, mitandao ya kijamii na huduma za kifedha kwa mtandao yakiongezeka kutoka miamala ya Sh bilioni 349.9 hadi Sh bilioni 366.1 Septemba mwaka huu.

Katika ripoti ya utendaji wa sekta ya mawasiliano kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2022/23, iliyotolewa na mamlaka hiyo imeonesha kuwa idadi ya laini za simu zinazotumika hadi kufikia Septemba mwaka huu ni milioni 58.1 kutoka milioni 56.2 Juni mwaka huu.

Takwimu zinaonesha kuwa Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha , Mbeya na Tabora zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya laini zinazotumiwa na watu na zinazotumika kwa ajili ya mawasiliano kwa mashine.

Akitoa ripoti hiyo leo Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari amesema kuna ushindani mkubwa kati ya watoa huduma, kwani hakuna mtoa huduma mwenye zaidi ya asilimia 35 ya laini zilizosajiliwa.

Amesema kuwa watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka milioni 29.1 Juni 2022 hadi milioni 31.1, Septemba mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 6.7.

Dk Bakari amesema mwelekeo wa ongezeko la watumiaji wa intaneti, linaonesha kwamba kulikuwa na ukuaji wa takribani asilimia 17 kila mwaka, katika kipindi cha miaka mitano ambapo 2017, kulikuwa na watumiaji milioni 16.1 na mwaka 2021 waliongezeka kufikia milioni 29.1.

Pia alieleza kuwa matumizi ya intaneti yameongezeka kutoka wastani wa MB 6,037 kwa watumiaji Machi mwaka huu hadi MB 6,626 Septemba mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button