Latifa: Watanzania changamkieni fursa za biashara Iran

MKURUGENZI  Mkuu wa TanTrade Latifa Mohamed Khamis amewataka watanzania kuchangamkia fursa za biashara katika nchi ya Iran

Latifa ameyasema hayo leo Julai  Mosi, 2023 katika maonyesho ya Kimataifa ya Sabasaba ikiwa ni siku ya taifa la Irani,

Amesema ni wakati sasa wa watanzania kubadili uwelekeo kwa kuchangamkia fursa zilizopo Irani hususani katika sekta ya kilimo, afya, teknolojia na elimu.

“Katika sekta ya kilimo Tanzania tuna fursa za kupeleka Ufuta, ngano na mafuta, ni fursa nzuri ambayo wakulima wetu wanapaswa kuichangamkia.” Amesema Latifa na kuongeza

“Katika afya pia wenzetu wametuzidi vitu vingi, tumeshaongea na ubalozi wa Iran hapa nchini na wamekubali kuleta madaktari wao ambao kutakuwa na kambi maalum kubadilishana utaalamu wao na madaktari wetu, teknolojia wanazotumia na sisi basi hatimae tuweze kupiga hatua zaidi katika matibabu.”Amesema

Aidha, amesema Watanzania wafikirie Iran kwa ajili ya kufanya nao kazi, kwanza vizuri katika suala la huduma kwa wateja, gharama kufanya biashara Irani sio ghali, Dola 100 ukibadilisha unapata zaidi ya elfu Hamsini hivyo  watanzania wanapaswa kwenda kubadili upepo wa kibiashara.

“Hata katika masuaa ya elimu wenzetu wapo juu, afya wapo juu. Watanzania watumie fursa za uhusiano za uwekezaji kikamilifu na sisi tuwe na bidhaa bora, Iran ni waaminifu bidhaa zao zina ubora.

“Mfano umenunua friji lililotengenezwa Iran utakaa nalo mpaka wajukuu zako watazikuta tofauti na mengine baada ya miaka miwili limeharibika unaanza kununua lingine.” Amesema

Amesema, baada ya maonyesho ya 47 ya Sabasaba  kutakuwa na maonyesho malaum ya Tanzania na Irani, lengo likiwa ni kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Iran ili kubadilishana uzoefu na fursa baina yao.

Nae, Balozi wa Iran nchini Tanzania Balozi Hussein Behineh amesema uhusiano mzuri wa kidiplomasia kwa miaka 41 kati ya Tanzania na Irani, unafungua njia za kibiashara na uwekezaji katika kuinua uchumi wa pande zote mbili

Amesema, kiwango cha biashara kati ya Iran na Tanzania katika kipindi cha miaka miwili 2021-2022 kimeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma ya 2019-2020.

Amesema, katika kipindi cha miaka miwili ya 2021-2022, Iran imeiuzia Tanzania bidhaa za dola milioni 95 ambayo ni ongezeko la asilimia 15 ukilinganisha na miaka ya 2019-2020.

Balozi huyo wa Iran, amesema pia katika kipindi cha miaka miwili ya 2021-2022, Iran imeagiza bidhaa kutoka Tanzania za dola miliioni 35 ambazo zimeongezeka kwa asilimia 35 ukilinganisha na miaka miwili ya  2019-2020.

 

 

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button