Latra: Jamii ina mwamko matumizi ya tiketi mtandao

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesema jamii sasa ina mwamko mkubwa juu ya matumizi ya tiketi mtandao kwa kuwa matumizi yanaonekana kuwa makubwa kwa abiria wengi wanaosafiri.

Ofisa Mfawidhi wa Latra Nyanda za Juu Kusini, Omary Ayoub alibainisha hayo wakati maofisa wa mamlaka hiyo waliposhirikiana na polisi kufanya ukaguzi wa kushtukiza wa tiketi mtandao kwa mabasi ya masafa marefu kwenye kituo kikuu cha mabasi Mbeya.

“Hii ni wazi kuwa jamii imeipokea na kuelewa maana ya tiketi mtandao lakini pia na umuhimu wake. Tunaendelea kuwasihi abiria wetu wanaosafiri kila siku kuendelea kujifunza na kutumia tiketi hizi,” alisema.

Aliwashauri abiria wanaokutana na changamoto yoyote ya tiketi mtandao kutosita kuwasiliana na mamlaka husika ili waweze kupata ufumbuzi na kuendelea na safari zao bila usumbufu.

Aliwataka pia abiria kuhakikisha wanalipa nauli iliyopangwa na serikali na kuepuka vishoka wanaopandisha bei kiholela kutokana na tofauti kati ya abiria anayehitaji tiketi mtandao na yule anayehitaji ya kizamani ya karatasi ya vitabu.

Kwa upande wao abiria waliokuwa kwenye mabasi yaliyokaguliwa kituoni hapo walipongeza hatua ya serikali ya kuanza kutumia tiketi mtandao wakisema imeondoa usumbufu uliokuwepo awali wa kutumia gharama za usafiri kwenda kukata tiketi au kiti kimoja kuuzwa kwa watu zaidi ya mmoja na kusababisha ugomvi kati ya abiria na watoa huduma.

Mmoja wa abiria hao, Hashim Musa alisema ujio wa tiketi mtandao pia umesababisha kutozwa nauli zilizo na uhalisia tofauti na awali ambapo kila wakala walijipandishia na kusababisha abiria wa safari moja kusafiri kwa nauli tofauti pasipo kujielewa.

Naye dereva wa kampuni ya mabasi ya New Force, Uswege Mwandambo alisema kwa sasa abiria wengi wana uelewa wa tiketi mtandao tofauti na kipindi cha awali ambapo iliwasumbua na kujikuta wakipata wakati mgumu wanaposafiri.

Habari Zifananazo

Back to top button