Latra yabadilisha njia za mabasi kuboresha usafiri

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) Mkoa wa Dodoma imebadilisha njia za kupita mabasi ili kuboresha usafiri na kuwapa urahisi wananchi kufika kwenye maeneo ya huduma likiwemo Soko la Wazi la Machinga.

Akizungumza jana Ofisa Mfawidhi wa Latra Mkoa wa Dodoma, Ezekiel Emmanuel alisema kutokana na kukua kwa kasi kwa Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya serikali, imewalazimu kubadilisha njia za mabasi.

Emmanuel alisema njia za mabasi zilizobadilishwa ni pamoja na njia ya Bahi, Chuo cha Mipango, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na barabara ya Dar es Salaam.

Advertisement

Magari kutoka barabara ya Bahi pamoja na maeneo ya Chigongwe, Kigwe sasa zitaishia katika Soko la Wazi la Machinga na kushusha na kupakia abiria nyuma ya soko hilo na kurudi njia hiyo hiyo.

Wakati mabasi kutoka njia ya Mpunguzi na Mlowa nayo yatashusha na kupakia abiria nyuma ya Soko la Wazi la Machinga kwa nyuma na kurejea njia hiyo.

Mabasi kutoka Udom yatafika Soko la Wazi la Machinga kupitia Hospitali ya General, Independence Square, Soko la Majengo na kurudi njia hiyo hiyo.

Vilevile mabasi kutoka njia ya Nanenane na Dar es Salaam yatapita Soko la Sabasaba kwenda kati ya Jiji na kupitia Hospitali ya General, Soko la Majengo, mzunguko wa Bahi, mzunguko wa Airport na kurudi.

Pia mabasi kutoka njia ya Mipango, St Gema, Msalato na Veyula yatapita mzunguko wa Airport kushusha abiria Soko la Wazi Machinga kupita mzunguko wa Bahi, Soko la majengo na kurudi.

Emmanuel alisema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha usafiri kati ya jiji na kuhakikisha wananchi wanafika kwenye masoko kupata huduma mbalimbali hasa soko jipya la Machinga.

Emmanuel aliwaalika wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika sekta ya usafiri hasa kwa kununua mabasi yenye kubeba abiria wengi hasa costa badala ya hiace ambazo mkakati wao ni kuziondoa barabarani.