LATRA yatangaza bei Daraja la Kawaida SGR

Dar - Dodoma Sh 31,000

DODOMA – Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza nauli za abiria wa daraja la kawaida kwa Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora ambapo abiria anayetoka Dar es Salaam hadi Dodoma atapaswa kulipa Sh 31,000. 

Kiasi hiki ni chini ya gharama ambazo mabasi mengi yanatoza kwa safari kama hiyo. Bei ya chini kwa basi kama la Shabiby ni Sh 29,000. 

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, Salum Pazzy amesema tangazo hilo linafuatia maamuzi ya Bodi ya Wakurugenzi kuhusu maombi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali.

“Kwa kuanza safari za SGR kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora, masharti muhimu yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya kutumika kwa nauli hizi ni pamoja na: TRC kuwa na leseni ya usafirishaji, ithibati ya usalama wa miundombinu ya reli na mabehewa, matumizi ya mfumo wa utoaji wa tiketi za kielekroniki, na kuunganisha mfumo huo na mifumo ya LATRA,” imesema taarifa ya LATRA.

Salum amesema katika taarifa kuwa, Mamlaka imelitaka Shirika kukokotoa malipo na utunzaji wa taarifa za abiria na nauli zilizolipwa, na kuwa na watumishi wenye ujuzi wa kutosha na madereva waliosajiliwa na LATRA.

Latra pia imetangaza nauli kwa watoto kuanzia umri wa miaka 4 hadi 12 ambapo nauli itakayolipwa kwa safari ya Dar es Salaam ni Sh 15,000.

SOMA: Njia tatu umeme wa uhakika SGR

Mtoto mwenye umri chini ya miaka minne hatalipa nauli, lakini taarifa zao zitahifadhiwa kwenye mfumo wa taarifa za abiria.

Masharti mengine ni kwamba TRC itapaswa kuweka mfumo wa usimamizi wa utoaji taarifa kwa wasafiri (Passenger Management Information System) na mfumo wa ufuatiliaji wa mwenendo wa treni (Train Tracking System), kuweka nauli za safari ya kituo kwa kituo katika maeneo yanayoonekana na abiria kwa urahisi.

Latra imesema mto huduma anapaswa pia uwepo wa huduma bora kwa wateja ikiwemo mazingira ya vituo (stesheni), usafi wa mabehewa, chakula na vinywaji, maji safi na salama, mwanga wa kutosha, na kuweka utaratibu wa fidia dhidi ya majanga na upotevu wa mizigo ya abiria.

Image

 

Habari Zifananazo

Back to top button