“Lengo la Serikali ni kuongeza ushiriki wa Watanzania sekta ya madini”

MWANZA: WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amezitaka Taasisi za fedha kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi(TPSF) na Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini(CTI) kuweka mpango wa kuwawezesha Watanzania kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa zenye uhitaji mkubwa migodini badala ya kuagiza bidhaa nje ya nchi na kuipotezea nchi mapato makubwa.

Mavunde ameyasema hayo leo Jijini Mwanza katika kikao maalum kati ya Wizara ya Madini na watoa huduma kwa Wamiliki wa Leseni kwa lengo la kujadiliana namna bora ya uwezeshwaji watanzania kushiriki katika uchumi wa madini.

“Dhamira ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuongeza ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini, mapato ya nchi kuongezeka na kuwa sekta inayoongoza katika mchango katika uchumi wa nchi.

Amesema, tangu kufanyika mabadiliko ya sheria ya madini ya mwaka 2017 na utungwaji wa kanuni za ushiriki wa Watanzania za mwaka 2018,idadi ya ushiriki wa Watanzania kwenye sekta ya madini imeongezeka kwa kiwango kikubwa tofauti na awali ambapo mpaka sasa zaidi ya watoa huduma 750 wamesajiliwa.

“Nia ya Serikali ni kuona watoa huduma wanawezeshwa ujenzi wa viwanda ili kuzalisha bidhaa bora nchini badala ya kuagiza bidhaa nje ya nchi, ” amesema.

Amesema, zaidi ya Sh Trilioni 2 zinatumika kila mwaka kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa na huduma mbalimbali migodini.

*Lazima fedha hizi zionekane katika uchumi wa Tanzania na kuchochea ukuaji wa mapato ya nchi na mtu mmoja mmoja,”amesema na kuongeza

” Nitoe rai kwa Taasisi za Fedha kuwawezesha watanzania kimitaji ili waweze kushiriki katika Uchumi wa Madini,” Amesisitiza Mavunde

Awali, akielezea mafanikio ya utekelezaji wa Kanuni za Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini za mwaka 2018, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba ameeleza kuwa ni pamoja na ongezeko la ajira kwenye migodi kutoka 6,668 kati ya 7,003 ikiwa ni asilimia 95 mwaka 2018 hadi kufikia 16,462 kati ya 17,024 sawa na asilimia 97 kwa mwaka 2022.

Aidha amesema ongezeko la manunuzi ya huduma na bidhaa kwa kampuni za kitanzania ni kutoka Dola za Marekani milioni 756.63 ambayo ni sawa na asilimia 62 ya manunuzi yaliyogharimu kiasi cha Dola za Marekani Milioni 1,228.38 kwa mwaka 2018 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.08 ambayo ni sawa na asilimia 86 ya kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.25 ya manunuzi yote yaliyofanyika mwaka 2022.

Akitoa salamu za awali,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CPA Amos Makalla amesema mkoa umejipanga kuweka mazingira wezeshi kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi kwenye madini ili kuongeza wigo mpana kwa watoa huduma kushiriki.

Habari Zifananazo

Back to top button