Leo ni bajeti ya kukuza uchumi

SERIKALI leo inatarajia kuwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 203/24 ikiwa na malengo sita ya uchumi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ametaja malengo hayo kuwa ni kuongeza kasi ya ukuaji wa pato halisi la taifa kufikia asilimia 5.2 mwaka huu kutoka matarajio ya ukuaji wa asilimia 4.7 mwaka mwaka jana.

Malengo mengine ni kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3 hadi 5 katika muda wa kati na mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya halmashauri) yafikie asilimia 14.9 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24.

Dk Mwigulu alisema hayo bungeni Dodoma Machi mwaka huu wakati anawasilisha tathmini ya utekelezaji wa bajeti katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu na mapendekezo ya mfumo na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Alitaja malengo mengine ya uchumi ni mapato ya kodi yafike asilimia 12.1 ya Pato la Taifa mwaka 2022/23 kutoka matarajio ya asilimia 11.5 mwaka 2022/23, kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti haizidi asilimia tatu ya Pato la Taifa na kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 ililenga kuongeza kasi ya kufufua uchumi na kuimarisha sekta za uzalishaji kwa ajili ya kuboresha maisha.

Misingi ya bajeti ya 2023/24

Dk Mwigulu alitaja misingi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 ni pamoja na kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara na kuendelea kuhimili athari za majanga ya asili, yasiyo ya asili na mabadiliko ya tabianchi.

Alitaja misingi mingine ya bajeti ni kuendelea kuhimili athari zitokanazo na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia na kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma katika soko la dunia.

Dk Mwigulu alitaja msingi mwingine wa bajeti mpya ni kuendelea kuimarika kwa utoshelevu wa chakula nchini na uwepo wa amani, usalama, umoja na utulivu wa ndani na nchi jirani.

Makusanyo

Dk Mwigulu alilieleza bunge kuwa kwa kuzingatia sera za bajeti kwa mwaka 2023/24 Sura ya Bajeti inaonesha kuwa Sh trilioni 44.38 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho sawa na ongezeko la asilimia 7.0 ikilinganishwa na bajeti iliyoidhinishwa na bunge ya mwaka 2022/23 ya Sh trilioni 41.48.

Alisema jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 31.38 sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote.

Dk Mwigulu alisema kati ya mapato hayo, yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 13.0 hadi Sh trilioni 26.72 kutoka makadirio ya Sh trilioni 23.65 mwaka wa fedha 2022/23.

Alisema misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo inatarajiwa kufikia Sh trilioni 5.46 sawa na asilimia 12.3 ya bajeti yote.

Malengo ya sera za mapato

Alisema sera za mapato na hatua za kiutawala kwa mwaka wa fedha 2023/24 zitalenga kuongeza makusanyo ya mapato kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini katika sekta za uzalishaji ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kuongeza wigo wa mapato.

Sera hizo pia zitalenga kuimarisha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na serikali itarekebisha sheria za kodi kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuongeza uwekezaji ili kuongeza mapato na itadhibiti misamaha ya kodi ili isizidi asilimia moja ya Pato la Taifa.

Dk Mwigulu alisema serikali pia itafanya tafiti na tathmini zinazolenga kuibua fursa mpya za mapato ya kodi na yasiyo ya kodi na kuendelea kuimarisha mifumo ya mashirika, taasisi za umma na wakala za serikali ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha gawio na michango stahiki inawasilishwa mfuko mkuu kwa wakati.

Kwa upande wa Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Humphrey Moshi ameishauri serikali itangaze bajeti yenye kuakisi maendeleo ya wote na iweke mazingira kuwezesha kila mtu awe na jukumu la kuchangia kulipa kodi.

Profesa Moshi anaishauri serikali itafute misaada ya nje na mikopo ambayo ina riba ndogo na muda wake wa kulipa utakuwa mrefu na pia iangalie namna ya kutumia fedha nyingine badala ya dola za Marekani ili kupunguza madeni na mfumuko wa bei.

Mshauri wa masuala ya uchumi na biashara kutoka Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye viwanda na Kilimo (TCCIA), Nebart Mwapwele anasema wanatarajia bajeti ya serikali ya mwaka 2023/24 itaakisi maoni na matarajio ya wengi katika biashara, viwanda na kilimo.

“Tumependekeza kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ipunguzwe hadi asilimia 15 kutoka 18, kuondoa ushuru kwenye mazao na kodi katika biashara zinazoanza ziondolewe kabisa hivyo tunatamani vionekane kwenye bajeti na tunaamini yataleta tija,” alisema Mwapwele.

Mbunge wa Bunda Boniphace Getere (CCM) anasema, wanatamani kuona bajeti yenye nafuu ya kodi kwenye vifaa na vitendea kazi vitakavyotengeneza fursa hasa kwa vijana wanaoendesha maisha yako kwa kuendesha bajaji na bodaboda.

Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje (Chadema) alisema “Serikali iwasilishe bajeti inayopunguza mzigo wa kodi na tozo kwa wananchi wa kipato cha chini kwani wananchi wamekuwa wakiumizwa nazo pamoja na kuwa ni shilingi 100 au 200 kwao hizo ni nyingi kutokana na hali ya maisha yao”.

Habari Zifananazo

Back to top button