Les Wanyika yarejea baada ya miaka 50

LES Wanyika ambayo ndiyo Bendi maarufu zaidi katika eneo zima la Afrika Mashariki, inarejea tena Tanzania ambako ilizaliwa rasmi miaka zaidi ya 50 iliyopita na kufanya tamasha la kwanza katika jiji la Arusha.

Kiongozi wa bendi hiyo, Sijali Zuwa, ambaye ni mzaliwa wa Morogoro, anasema bendi hiyo imekuwa ikifanya shughuli zake za muziki nchini Kenya kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita.

“Sasa kwa mara ya kwanza baada ya miongo kumi, tangu iondoke nchini Les Wanyika inarejea nyumbani ilikozaliwa na kufanya maenesho katika viwanja vya Via-Via, jijini Arusha.”

Advertisement

Tayari Les Wanyika wamefanya onesho la kwanza jijini Arusha na sasa wanajipanga kufanya kuvamia tena jukwaa siku ya Jumamosi ya tarehe 27, June 2023, kwa mujibu wa Meneja wa bendi Boni Nyaga.

Maonesho ya Les Wanyika nchini ni sehemu ya Tamasha la kimataifa la Utamaduni, Sanaa na Michezo la Afrika linalofanyika jijini Arusha kwa wiki nzima.

“Watu waje wapate ladha halisi ya Wanyika, maana wengi huwa wamezoea kusikia bendi zingine ziipiga kopi za nyimbo zetu,” aliongeza Nyaga.

Les Wanyika ni maarufu kwa nyimbo kama ‘Afro,’ ‘Nimaru,’ ‘Pamela,’ ‘Sina Makosa,’ ‘Kasuku,’ na ‘Safari ya Samburu.’

“Les Wanyika chimbuko lake in jijini Arusha, miaka ya mwanzo ya sabini lakini bendi ilianza ikijulikana kama ‘Arusha Jazz Band,’ na baadae ikahamia nchini Kenya ambako ilibadilisha jina na kuitwa Simba Wanyika,” alisema Zuwa.

Bendi ilianzishwa jijini Arusha miaka ya mwanzo ya 70 na ndugu wawili George na Wilson Kinyonga na ilipohamia Kenya ikapata umaarufu mkubwa nchini humo.

Mwaka 1978 baadhi ya wanamuziki wakiongozwa na Profesa Omar Shaaban walijiengua kutoka Simba Wanyika na kuanzisha Les Wanyika bendi ambayo ipo mpaka leo, na sasa imerejea katika eneo ilipozaliwa.

Hata hivyo kuna kipindi bendi ilisitisha muziki kwa takriban miaka 24 kabla ya kurejea tena kwenye fani mwaka jana.

Wanyika, ingawa ilijulikana duniani kote kama bendi ya Kenya, lakini wanamuziki wake wengi walikuwa ni watanzania, asilimia kubwa wakitokea mkoani Tanga, wakiwemo kina Issa Juma, Omari Shaaban na John Ngereza.

Hata waanzilishi, akina Kinyonga chimbuko lao ni jijini Tanga ambako awali walikuwa na kundi maarufu la Jamhuri Jazz.

1 comments

Comments are closed.