WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana ametoa rai kwa balozi za Tanzania nje ya nchi ziwawasilishe takwimu za walimu wanaohitajika kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi wanazowakilisha.
Dk Chana ametoa rai hiyo Februari 22, 2023 alipofanya ziara ya kwanza katika Ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.
Akizungumza katika ofisi hizo, Waziri huyo ameitaka BAKITA kuendelea kuwa na matukio mengi ikiwemo makongamano, warsha mikutano na majukwaa mbalimbali ya kuendeleza na kubidhaisha lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi.
“Nampongeza sana Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika mikutano ya kimataifa ikiwemo ya Umoja wa Afrika na Afrika Mashariki, pamoja na kuongeza bajeti katika kubidhaisha lugha hii adhimu,” amesema Waziri Chana.
Ameielekeza BAKITA ishirikiane na vyuo vikuu vyenye vitivo vya lugha ya Kiswahili katika kuandaa wataalamu wa lugha hiyo, ili kuongeza ufundishaji wa lugha hiyo kwa ufasaha.
Awali Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Pauline Gekul akizungumza wakati wa kumkaribisha Waziri Chana, alilipongeza baraza hilo kwa kuendelea kutekeleza vyema mkakati wa wa miaka kumi wa kubidhaisha Kiswahili ulioanza mwaka 2022 hadi 2032.