Lewandowski aionya Bayern
MUNICH, Ujerumani; Mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski ameionya klabu yake ya zamani ya Bayern Munich kwamba Real Madrid “inashinda michezo ambayo huwezi kuamini”
Lewandowski ameyasema hayo alipozungumza na mtandao wa Sport BILD wa Ujerumani ikiwa ni kuelekea mchezo wa hapo baadaye wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ambapo wababe hao wa jiji la Munich watakuwa nyumbani Allianz Arena kuwakaribisha Los Blancos katika mechi ya mkondo wa kwanza wa Nusu Fainali ya ligi hiyo pendwa Duniani.
“Ni mchezo muhimu sana kwa Bayern baada ya msimu mgumu kama huu, Wana nafasi ya kutinga fainali. Hata hivyo, ni kazi kubwa, utakuwa ni mchezo wa 50 kwa 50”
“Huwezi kamwe kuwadharau Real Madrid. Wanashinda mechi ambazo huwezi kuamini, huwezi kuelezea. Real Madrid hawafi kamwe. Hawakati tamaa. Wanacheza kama timu uwanja mzima. Wakati mwingine unaweza kudhani unakaribia kushinda, lakini mwishowe hushindi”.
“Hata hivyo Bayern wana nafasi, lazima wafanye vizuri katika mechi hii ya nyumbani, mechi ya Bernabeu ni tofauti mambo mengi ya nje ya pitch yanaweza kuamua mchezo hili nimelijua hivi punde. Natamani Bayern waifunge Real Madrid, nawaombea” alimaliza
Lewandowski aliifungia Bayern mabao 344 katika mechi 375, kabla ya kujiunga na Barca msimu wa majira ya joto wa 2022. Ikumbukwe kuwa hivi karibuni timu yake ya Barcelona ilichapwa 3-2 na Madrid kwenye El Clasico bao la dakika za jioni dakika za kutoka kwa Mwingereza Jude Bellingham.