LHRC yampongeza Samia uboreshaji haki jinai

LHRC yampongeza Samia uboreshaji haki jinai

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuona mfumo wa haki jinai unaboreshwa kwa lengo la kufanya mageuzi katika utoaji wa haki.

Akizungumza na waandishi wa habari J umatano jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema kituo kimekuwa mstari wa mbele  katika kupigania na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha na kufumua mfumo mzima wa haki jinai ili kuendana na mazingira.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kulinda haki za binadamu hususani haki za mahabusu na kulinda haki za watu wanaowategemea.

Advertisement

“Tumekuwa tukipigania kuboreshwa mfumo wa haki jinai mbalimbali kwa kutoa ripoti maalumu ya kila mwaka, kufungua mashauri mbalimbali mahakamani, kufanya uchambuzi na kuwasilisha miswada bungeni pamoja na kukutana na wafanya maamuzi. Ikumbukwe hii si kauli ya kwanza ya Rais Samia kuhusiana na masuala ya haki jinai,” alisema.

Wakati akifungua kikao cha maofisa  waandamizi wa polisi, mkoani Kilimanjaro, Samia alikemea tabia ya baadhi ya askari polisi kuwabambikizia kesi wananchi na kutoa mfano wa kufutwa kesi 1,840 ambazo wananchi walikuwa wamebambikiwa.