Ligi Kuu Bara haipoi

Ligi Kuu Bara haipoi

LIGI Kuu Soka Tanzania Bara unaweza kusema haipoi kutokana na mwenendo wa kila timu, tofauti ndogo ikimpa nafasi mwingine kupanda na kushuka kupishana nafasi.

Wiki iliyopita, Yanga ilikuwa inaongoza, lakini wiki hii tofauti ya mabao wanashushwa hadi nafasi ya pili na watani zao wa jadi Simba, ambao sasa wanashika usukani.

Simba na Yanga baada ya kucheza mizunguko mitano kila mmoja zinalingana pointi sawa 13, sare moja kila mmoja, hazijapoteza na zote zimefunga mabao 11 ila utofauti wao ni mabao ya kufungwa, ambapo Yanga imeruhusu manne na Simba mawili.

Advertisement

Timu hizi hazipoi zote ni bora isipokuwa mtazamo wa wengi wanaona Yanga ina safu bora ya ulinzi, lakini ndiyo iliyoruhusu mabao mengi dhidi ya mwenzake Simba.

Washambuliaji wao tegemeo ni Moses Phiri wa Simba, ambaye kila mechi amekuwa akifunga kuonesha wazi ni mchezaji hatari na mpaka sasa ana mabao manne, huku Mayele wa Yanga akiifungia timu yake mabao matatu.

Kwa mwenendo huo mzuri kwa wakongwe hao, unaonesha ushindani ni mkali ila kuna presha mbele ikiwa mmoja atapoteza au kupata sare kwa sababu hakuna anayetaka kuachwa mbali na mwenzake kwa tofauti ya pointi.

Namungo imeonesha uhai tena baada ya kuyumba misimu miwili iliyopita wamerudi kivingine, sawa na Azam FC ambao wamesajili vizuri na ushindani waliouonesha kwenye mechi zilizopita wako kwenye mstari mzuri.

Mshambuliaji wake, Reliants Lusajo bado ni bora na ndiye kinara akiongoza kwa kufunga mabao matano.

Pointi 11 za Namungo na Azam FC wako sambamba na vinara wa juu kwa tofauti ya pointi mbili hivyo bado kazi mbichi.

Kuna timu kama Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar ambazo msimu uliopita zilikuwa zimeyumba kwa kuanza vibaya nazo zimeonesha uhai japo kidogo huku Singida Big Stars iliyopanda ikiwa tishio kwa kuleta ushindani kutokana na kusajili wachezaji wengi wazuri.

Kuna wengine kama Tanzania Prisons, Coastal Union na KMC ambao ni timu zisizotabirika, kuna wakati zinajitahidi na muda mwingine utaziona ziko chini bado mapema huenda kadiri siku zinavyokwenda zikaonesha taswira mpya.

Msimu uliopita timu zilizoanza vyema kama Mbeya City, Dodoma na Geita Gold na Kagera Sugar, awamu hii mambo magumu huenda zikabadilika baadaye kwani nafasi walizopo si nzuri.

Geita imetoka kushinda mchezo wake wa kwanza uliopita dhidi ya Polisi Tanzania, huku mshambuliaji wake, George Mpole akianza kurejea taratibu baada ya kufunga jumla ya mabao mawili katika michezo mitano.

Ihefu bado mambo magumu kama mwaka juzi, wameshindwa kupata ushindi wowote huenda baada ya kumwongeza kocha Juma Mwambusi atasaidia mabadiliko.

Mchezo wao uliopita dhidi ya Tanzania Prisons walipata sare ya kwanza tangu waanze ligi.