Ligi Kuu Bara kutimua vumbi Agosti 15

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa Kalenda ya Matukio ya msimu mzima wa 2023/24 inayoyasimamia ikionesha msimu mpya wa Ligi Kuu Bara utaanza Agosti 15, mwaka huu.

Kalenda hiyo imeonesha kufunguliwa kwa pazia la usajili Julai 1, 2023 ambalo linahusisha timu za madaraja yote kuanzia Ligi Kuu, Championship, Ligi Daraja la Kwanza na Michuano ya FA na zoezi hilo litafungwa Agosti 31.

Kalenda hiyo pia imejumuisha tarehe za kuanza kwa michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mechi za awali zimepangwa kuanza Agosti 18 na 20, 2023.

Advertisement

Ligi ya Championship imepangwa kuanza Septemba 2, 2023, wakati Ligi Daraja la Kwanza yenyewe ikipangwa kuanza Oktoba 21, 2023, pia kuanzia Agosti 1 hadi 7 ni wakati wa semina maalumu na utimamu wa mwili pamoja na kujikumbusha baadhi ya sheria na kanuni kwa waamuzi watakaochezesha ligi hizo.

Kuanzia Agosti 1-15, 2023 itakuwa ni kipindi cha usajili kwa timu zinazoshiriki michuano ya Caf, ambapo Agosti 4 itakuwa siku maalumu kwa Shirikisho la soka nchini, TFF na Bodi ya Ligi kutoa semina kwa waandishi watakaoripoti michuano hiyo.

Katika upande wa mashindano ya kimataifa kwa timu za Taifa Julai 28 hadi 30 ligi itasimama kupisha mechi za mkondo wa kwanza kufuzu fainali za Chan ambayo mechi za marudiano zimepangwa kupigwa Agosti 4 hadi 6, 2023, mechi za michuano hiyo zitaendelea tena kwa hatua zinazofuata kuanzia Septemba 1 hadi 3.

Septemba 4-12, itakuwa ni kipindi cha mechi za kirafiki za kimataifa zilizopo kwenye kalenda ya Fifa na tarehe hizo hizo ndani ya mwezi huo ndipo mechi za kuwania kufuzu fainali za Afcon zitakazofanyika nchini Guinea 2025, zitachezwa.

Kwa mujibu wa Kalenda hiyo msimu wa 2023/24 unatarajia kumalizika Juni 9 kwa mchezo wa mtoano kwa timu ambazo zimemaliza nafasi ya 13 na 14 kwenye Ligi Kuu pamoja na Championship wakati katika upande wa mashindano ya kimataifa msimu utahitimishwa kwa mechi za kufuzu Kombe la Dunia mechi zikichezwa Juni 03 hadi 11.