NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ameagiza makampuni na maeneo yanayotumia kazi za Sanaa na ubunifu kujinufaisha kibiashara kuhakikisha yanalipa mirabaha na madeni ya nyuma yanayodaiwa.
Hamis Mwinjuma ametoa maagizo hayo leo Machi 16, 2023 alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kwa ajili ya kujionea shughuli zinazofanywa na ofisi hiyo ambapo ameiagiza Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) iwachukulie hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani wote waliokaidi kulipa.
Hatua hiyo inakuja baada ya COSOTA kuwasilisha taarifa inayoonesha kuwa baadhi ya makampuni nchini yamekuwa yakikaidi kwa makusudi kulipia mirabaha huku yakiendelea kutumia kazi za Sanaa katika biashara zao.