MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD) nafasi atakayoihudumu kwa mwaka mmoja na kuahidi kusimamia kuongeza maridhiano na ushirikiano.
Lipumba amechukua kijiti hicho, akimpokea Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahaman Kinana aliyekuwa akishika nafasi hiyo, huku Haji Ambar Khamis wa NCCR Mageuzi akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa TCD.
Uchaguzi huo umefanyika katika mkutano mkuu wa TCD uliofanyika Dar es Salaam jana, ambako pia walijadili masuala mbalimbali ya utekelezaji wa mipango ya kituo hiko kwa mwaka 2023/2024.
Miongoni mwa yaliyojadiliwa ni mabadiliko ya katiba ya TCD na maandalizi ya kongamano la demokrasia ambalo linatarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Akielezea vipaumbele vyake, Profesa Lipumba amesema atasimamia kuongeza maridhiano na ushirikiano kama ambavyo mtangulizi wake amefanya.
“Malengo ni kuhakikisha Tanzania inasonga mbele katika Ujenzi wa demokrasia ya kweli, inakuwa nchi tulivu na iwe chombo au nyenzo ya kujenga uchumi shirikishi kazi ambayo ni ya Watanzania wote na sisi tunaendeleza kazi hiyo,” amesema Profesa Lipumba.
Pia Prof. Lipumba amesema atasimamia kujenga mazingira mazuri uchaguzi wa serikali wa mitaa utakaofanyika mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 uweze kuwa wa huru na wa haki.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti mpya wa TCD, Haji Ambar Khamis ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, amesema wameridhika na hali ya kisiasa ilivyo sasa nchini ikiwemo kuruhusiwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na maridhiano baina ya vyama.
Comments are closed.