UDUMAVU kwa mtoto pamoja na lishe duni, huchangia kupata athari zisizoweza kurekebishwa katika maisha yake yote, hata kama baadaye atapata lishe bora.
Pia udumavu kwa kiasi kikubwa husababisha kupungua kwa kasi ya maendeleo ya ukuaji wa akili ya mtoto, hali inayosababisha watoto kupata matokeo duni kielimu kutokana na lishe duni waliyoipata wakiwa wadogo.
Hayo yamesemwa leo na Ofisa Lishe Mkoa wa Arusha, Rose Mauya, wakati wa maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika wilayani Arumeru, mkoani Arusha.
Amesema endapo watoto wakiwa na lishe duni wanapata athari mbalimbali katika ukuaji wao, hivyo kusababisha kupata matokeo duni ya kielimu.
Amesema hali ya upatiamlo kwa Mkoa wa Arusha ni asilimia 25, huku Kitaifa ikiwa ni asiliamia 34, hivyo alitoa rai kwa wakulima kulima mazao yatakayopunguza tatizo la lishe na utapiamlo yanayosababisha udumavu kwa watoto.
Kwa upande wake Mtafiti wa Uboreshaji Mbogamboga kutoka World Vegetable Center, Fekadi Dinssa, amesema mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo janga la Covid-19, yamechangia kwa asilimia kubwa masuala ya lishe.
Amesema mtazamo wa kituo chao ni kuhakikisha aina mbalimbali za mboga zinazalishwa, ili kuongeza virubitubisho na kuongeza uzalishaji wa chakula.