Lishe duni sababu wanafunzi kuchukia hisabati
MBEYA; LISHE duni kwa watoto imetajwa kuwa miongoni mwa sababu za ufaulu hafi fu wa masomo ya sayansi na hisabati kwa wanafunzi nchini kwani waliokosa lishe bora huwa na uelewa mdogo darasani wanapofundishwa.
Aidha, imeelezwa asilimia kubwa ya watoto wenye lishe duni huyakwepa na kuyachukia masomo hayo wakiyaona ni magumu kwa sababu yanahitaji uwezo mzuri wa kufikiri.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Ofisa Lishe wa Jiji la Mbeya, Itika Mlagalila kwenye kongamano la kuimarisha ufaulu na ustawi wa wanafunzi shuleni kupitia lishe toshelevu lililoandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la HELVETAS.
Itika alisema watoto waliokosa lishe bora huwa na uelewa mdogo darasani wanapofundishwa na wakati mwingine huchukia kwenda shule na kuanza utoro hali inayowafanya wazorote zaidi kielimu.
Isome pia: https://habarileo.co.tz/changamoto-somo-la-hisabati-kupatiwa-ufumbuzi/
“Masomo ya sayansi na hisabati si magumu ila yanahitaji uwezo wa kufikiri hivyo utafiti unaonesha watoto wenye lishe duni huwa wanayachukia zaidi masomo haya sababu hawana uwezo mzuri wa kufikiri kwa hiyo suala la lishe linaathiri mpaka ufaulu kwa watoto wetu,” alisema.
Naye Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya, Yesaya Mwasubila alisema wamebaini utaratibu wa wanafunzi kula chakula cha mchana shuleni una kasoro mbalimbali kutokana na aina ya chakula kinachoandaliwa kwenye shule hizo.
Alisema shule nyingi watoto wanakula makande na walipowahoji walimu walisema chakula hicho ndicho kinapatikana kirahisi na kwa bei nafuu hali ambayo alisema si sahihi na badala yake wanatakiwa kuwaandalia watoto chakula bora.
Alisema chakula ambacho watoto wanastahili kukipata ni chenye mchanganyiko wa makundi sita ambayo ni wanga, mafuta, sukari, matunda, mboga na vyakula vya asili ya wanyama na hivyo wanaendelea kutoa elimu kwa wadau ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki kuimarisha lishe ya watoto shuleni.
Ofisa Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Chakula Jiji la Mbeya kutoka HELVETAS, Judith Sarapion alisema mradi huo unatekelezwa kwa miaka mitatu na tayari wameshazifikia kata zote 36 za Jiji la Mbeya kuelimisha upatikanaji wa lishe bora kwa wanafunzi shuleni kwa kuwahamasisha wazazi kuchangia chakula na kuhamasisha upandaji wa bustani shuleni.
Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa aliwataka wadau wote wakiwemo viongozi wa dini kushiriki kuhamasisha uchangiaji wa chakula shuleni kwa kuwa ni utekelezaji wa sera ya elimu.