DAR ES SALAAM; MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango, amesema miongoni mwa vipaumbele alivyopigania hayati Edward Lowassa ni elimu.
“Alikuwa kinara wa vipaumbele vitatu vya kitaifa, na kwa hili sitasahau kwenye kikao kimoja alipoulizwa juu ya vipaumbele alisema cha kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na cha tatu ni elimu, kwa sababu hiyo alisimamia kwa uhodari utekelezaji wa sera, mikakati na mipango mbalimbali ya elimu,” amesema Dk Mpango.
Dk Mpango amesema katika nafasi ya Waziri Mkuu, Lowassa alihimiza uhifadhi na utunzaji wa mazingira. Amesema kwa sababu hiyo iwe ukumbusho wa kutunza mazingira hasa vyanzo vya maji, ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunapomuaga leo (hayati Edward Lowassa), tujikumbushe wajibu wa kila mmoja wetu kwa nchi yetu na kuyaishi kwa vitendo mambo yote mazuri tunayojifunza kutoka kwenye maisha yake,”amesema Dk Mpango.
–